Shule ya Sekondari Viwandani yamshukuru Mbunge Mavunde kuboresha miundombinu ya Elimu

Na. Faraja Mbise, VIWANDANI

Uongozi wa Shule ya Sekondari Viwandani wamshukuru Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo sambamba na ujenzi wa maabara mpya ya kompyuta na ugawaji wa kompyuta 20, viti 20 na printa moja.



Shukrani hizo zilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Viwandani, Mwl. Ester Simchimba, alipokuwa akitoa taarifa ya shule hiyo katika hafla ya ugawaji Kompyuta na Printa kwa shule za sekondari jijini Dodoma, iliyofanyika tarehe 10 Machi, 2025 katika Shule ya Sekondari Viwandani, Kata ya Viwandani, jijini Dodoma.

Akisoma risala hiyo, Mwl. Simchimba alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwa mdau mkubwa katika kusimamia taaluma na kuboresha miundombinu ya shule hiyo, sambamba na kutoa nafasi ya kipekee ya kuichagua shule hiyo kuwa sehemu maalum kwa kufanyia tukio hilo la kihistoria katika shule hiyo. “Tunashukuru kwa kuchagua shule yetu kuwa mahali pa kufanyia hafla hii fupi na tukio la kihistoria katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikiwakilisha shule zote 50 za sekondari. Aidha, tunakushukuru sana kwasababu umekuwa mdau mkubwa katika kusimamia taaluma na kuboresha miundombinu lengo ikiwa ni kuongeza umahiri wa ujifunzaji na ufundishaji katika wilaya yetu” alishukuru Mwl. Simchimba.


Akizungumzia hali ya taaluma na ufaulu wa wanafunzi shuleni hapo, alisema kuwa wameona mchango wa Mbunge wa Dodoma Mjini katika kuboresha na kupandisha taaluma ya shule hiyo. “Viwandani Sekondari tumeona matunda ya mchango wako katika matokeo ya mitihani ya taifa kwa kidato cha Pili na Nne. Kwa mwaka 2024 tumepata tuzo ya ubora wa matokeo na zawadi kwa kuwa nafasi ya kwanza kwa matokeo ya kidato cha Pili. Pia tumepata tuzo kwa kuwa nafasi ya tatu katika matokeo ya kidato cha Nne kwa shule za sekondari jijini Dodoma na kufuta zero kwa matokeo ya kidato cha Nne” alisema Mwl. Simchimba.

Sambamba na hilo, alimshukuru Diwani wa Kata ya Viwandani, Japhary Mwanyemba kwa mchango mkubwa alioufanya katika kuhakikisha maboresho mbalimbali ya shule hiyo kwa kuishirikisha Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatenga fedha kwa ajili ya maboresho hayo. “Tunamshukuru Diwani wa Kata ya Viwandani kwa kuwa mlezi namba moja wa kata hii, yeye ni sehemu ya wadau wakubwa waliochangia ujenzi wa uzio, amekuwa mstari wa mbele kuchangia chakula wakati wa kambi za taaluma hapa shuleni. Pia shule hii ina miradi mingi ambayo amepambana na kuishirikisha halmashauri kuhakikisha fedha zinaletwa hapa shuleni” alishukuru Mwl. Simchimba.



Shule ya Sekondari Viwandani ilianzishwa Mwaka 2006 na ina jumla ya wanafunzi 939 ambapo idadi ya wavulana ni 462 na wasichana 477. Aidha, shule ina jumla ya walimu 47 (wanawake 33 na wanaume 14).

MWISHO

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma