Mbunge Mavunde agawa Kompyuta na Printa Shule za Sekondari za Serikali Dodoma

Na. Leah Mabalwe, VIWANDANI

Wanafunzi wa shule za sekondari za serikali waaswa kuongeza jitihada katika masomo yao ili kuzidisha ufaulu.



Hayo yalisemwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde wakati wa hafla ya ugawaji wa komputa na printa katika shule zote za serikali za sekondari jijini Dodoma na uzinduzi wa maabara ya kisasa ya kompyuta ya Shule ya Sekondari Viwandani.

“Napenda kuhamasisha wanafunzi wote wa shule za sekondari kuongeza jitihada sana katika masomo yenu. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sasa anawekeza sana katika sekta ya elimu ili wanafunzi wote mpate mazingira mazuri kwa ajili ya kujisomea. Kwa sasa tunahitaji kujenga Jiji la Dodoma katika sekta ya elimu na kazi kubwa bado zinaendelea kufanyika. Nimeamua kufanya ziara hii ya ugawaji wa kompyuta katika shule zote za Dodoma mjini ili kuwaongezea maarifa pamoja na kukua kwa utandawazi kwasababu tunarahisisha upataji wa maarifa kwa ninyi wanafunzi wote. Kompyuta hizi zina kila kitu ambacho wanafunzi mnahitaji kujifunza. Hivyo, niwasisitize sana kuongeza juhudi katika masomo yenu” alisema Mavunde.



Akiongelea suala la watoto wenye ulemavu alisema kuwa nao wanafursa ya kupata elimu kama watoto wengine. “Na sitoishia hapa nina mpango pia wa kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu pamoja na watoto wenye ulemavu wa Jiji la Dodoma kwa kugawa madaftari bure pamoja na mabegi ya mgongoni, suala hilo lipo katika mchakato hivyo basi, serikali yetu kwa sasa imejipanga kikamilifu kukemea ubaguzi wa watoto wenye ulemavu” alisema Mavunde.

Nae, Mkuu wa Shule ya Sekondari Viwandani, Ester Simchimba alimshukuru Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mchango wao mkubwa wa kuboresha miundombinu ya shule hiyo.

“Tunakushukuru mbunge wetu kwa kufika katika shule yetu kwaajili ya hafla ya utoaji wa vifaa vya Kompyuta pamoja na printa lakini pia kwa ajili ya uzinduzi wa maabara ya kisasa. Kwa niaba ya uongozi wa shule pamoja na kamati ya wazazi tunakushukuru sana kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya shule yetu kwasababu umeshirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya shule na hata kupelekea kuongezeka kwa ufaulu mzuri kwa wananafunzi, tunakushukuru sana mbunge wetu” alisema Mwl. Simchimba.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma