Mikopo ya 10% yawanufaisha vijana wa Kata ya Ipala
Na. John Masanja, IPALA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma yakipatia kikundi cha Kazi iendelee Ipala mkopo usio na riba
wa shilingi 17,000,000 kwa ajili ya kuongeza mtaji kwa shughuli ya bodaboda na
kutengeneza ajira kwa vijana ili waweze kujitegemea kimaisha.
Hayo yalielezwa na Mhasibu wa Kikundi cha Kazi iendelee, Peter Mhaka mbele ya waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika kata hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
“Kikundi
kilipata mkopo huu ili kujikwamua kiuchumi. Mwaka 2023 tulichukua mkopo wa
shilingi 17,000,000 tukiwa watano, tukanunua bodaboda tano ambazo zimetunufaisha
kwa kusomesha watoto, tumejiingiza kwenye kilimo na tumepunguza utegemezi yote
hii ili kujikwamua zaidi kiuchumi” alisema Mhaka.
Aidha,
aliiomba serikali kuendelea kuhamasisha vijana ili wafahamu umuhimu wa mikopo
hiyo. “Nawashauri vijana wenzangu wachangamkie fursa ya mikopo hii isiyoumiza,
watembelee ofisi za kata ili kupata elimu ya mikopo hii” alisema Mhaka.
Nae Afisa Mtendaji wa Kata ya Ipala, Herman Malindila alikipongeza Kikundi cha Kazi iendelee na kuwasihi kuendelea kuchangamkia fursa zinazotolewa kwa vijana na serikali ya awamu ya sita. “Nawapongeza vijana kwa kazi nzuri, muendelee kuwa mfano kwa wengine ili nao waje waone umuhimu wa mikopo hii. Serikali yetu inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inajali vijana wa rika zote hivyo, changamkieni fursa ili kujikwamua kiuchumi” alipongeza Malindila.
MWISHO
Comments
Post a Comment