Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa
Na. Halima Majidi, DODOMA
Wananchi wa Kata ya Makutupora, jijini
Dodoma, wameeleza kilio chao juu ya changamoto kubwa zinazowakabili, zikiwemo
ukosefu wa maji safi, matatizo ya umeme, pamoja na shule kuwa mbali, hali
inayowakwamisha katika shughuli za kila siku.
Wakizungumza katika mkutano wa mkuu wa mkoa uliofanyika
katika Kata ya Makutupora, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema wamekuwa
wakikumbana na shida ya maji kwa muda mrefu, huku wakilazimika kutembea umbali
mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Akitoa kero hiyo, mkazi wa Mtaa wa Sekondari,
Pasisi James, alisema kuwa, tangu kuhamia katika mtaa huo ni miaka mingi hivyo
ameiomba serikali kuwasogezea huduma ya maji kwa sababu imekuwa ni changamoto
kubwa na hivyo kushindwa kuendelea na kazi zao za kila siku. “Maji ni tatizo
hapa kwetu, tunamiaka mingi tangu kuhamia hapa, nimekuja hata kusoma sijui
mpaka leo bado tunahangaikia maji, tunachukua maji kwa wachina dumu moja hilo
hilo ufulie pamoja na kunywa, hapo naomba mtusaidie” alisema.
Aidha, alieleza kuwa kwa upande wa shule
wanawatoto wadogo wa miaka mitano na shule inayotegemewa ni Makutupora na
Veyula, wanalazimika kutembea umbali mrefu. Hivyo, wanashindwa waandikisha
watoto kutokana na shule kuwa mbali. “Umbali wa shule, watoto wengi wanashindwa
kwenda shule kwa sababu hiyo. Hivyo, kungekuwa na uwezekano wa kupata gari kama
wenzetu wanavyofanya na ikapatikana mia mbili, mia tatu ili watoto waweze
kufika shuleni” alisema James.
Nae, Mkazi wa Makutupora, Victoria Madeje, alisema
mbali na changamoto ya shule kuwa mbali na watoto kushindwa kwenda shule, pia alilalamikia
uhaba wa huduma za umeme, wakidai kuwa baadhi ya maeneo bado hayajaunganishwa,
hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi hao. “Nimejaza fomu mara mbili
na sijawahi kupata umeme hata siku moja, hivyo tunashindwa kusaga hata chakula
tunatoka kisae tunakuja kusaga Veyula tunashida, tunaomba angalau watuletee
umeme watakao kuwa na uwezo watuletee mashine jamani hiyo ndio kero yetu mtaa
wa 36, sekondari mpaka kisae” alisema Madeje.
Kwa upande wake Ndeliani Richard alimshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada
wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuomba huduma iwe endelevu kwa sababu
inasaidia katika shughuli mbalimbali ikiwemo shamba na vifaa vya shule. “Tunaomba
iwe endelevu, tunaambiwa mwezi wa tisa mkataba unaisha, lakini tunaomba mama asituchoke,
tunaomba atusaidie bado wajukuu na watoto wengine wanasoma, tunafanya biashara
ndogondogo tunamshukuru sana kwa msaada wake” alisema Richard.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Dkt. Frederick Sagamiko akijibu kero hizo alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma
katika kuhakikisha inaunga mkono jitihada za kuwa kila mtoto anapata haki ya
elimu, ilitenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwaajili ya ujenzi wa shule ya
msingi mama katika Kata ya Makutupora, Mtaa
wa Sekondari, ambapo mpaka sasa pesa hiyo haijatumika popote kutokana na zuio
la eneo hilo, kwa sababu eneo lililotengwa kwaajili ya ujenzi wa shule hiyo ni
la bonde. “Wananchi wanatakiwa kuwa na subira, bado eneo lipo katika zuio ni
eneo la bonde nadhani kuna maelekezo yametolewa, ile kazi itakapokamilika Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, sisi tupo tayari wakati wowote kama tutaruhusiwa
kuendelea pale tutajenga, tutakuja tuone ‘plan B’ kama tunafanje kama hilo eneo
halitatumika” alisema Dkt. Sagamiko.
Sambamba na hayo, alielezea suala la kata
hiyo kutengewa eneo kwaajili ya makaburi kwamba eneo lililopo limejaa na kuna
maombi yaliofanywa na diwani wa kata kwa kuwasiliana na Magereza ambapo
wameomba ekari 50, na mpaka sasa Magereza wanaendelea kuchakata taarifa hiyo
kiofisi. “Wakikamilisha taratibu za kiofisi wataenda kutuonesha sisi Jiji tuje
tupime tayari kwaajili ya kutumika kwa maziko” alisema Dkt. Sagamiko.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyemula alikiri
kuwepo kwa changamoto hizo na kusema kuwa juhudi zinaendelea kufanyika na
ataendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa
suluhisho la kudumu, pia amefafanua kuwa malengo ya Mkoa wa Dodoma ni
kuhakikisha kila mwanadodoma anafurahia amani na utulivu na kuona kuwa kila mtu
anainuka kiuchumi. “Ili uinuke kiuchumi ndugu zangu sio lazima uwe unapata
fedha nyingi, wapo wanaopata milioni lakini hawana wanachokifanya inatka
maarifa na hekima, hekima ya kupima nifanye hiki badala ya hiki, hivyo naomba
hicho mnachokipata tuinuke kwenye uchumi” alisema Senyemule.
Sanjari na hayo aliwapongeza wananchi kwa
kuona juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwapatia wananchi fedha za kujikimu. TASAF ameamua kufanya hivyo
kwasababu huo ni utashi, aliongeza kuwa kwa wale wanaotaka miti ya maembe
watapewa mti mmoja mmoja, amewataka kuitunza kwa sababu miti hiyo imenunuliwa
kwa gharama. “Ameamua kuwa hawa ni wananchi wangu tuendelee kuwasaidia, ulizeni
nchi nyingine kama wanatoa tu fedha bila ya mtu kufanya kazi yoyote, kwa
kuangalia hali ya wananchi wake na kuwapatia fedha ya kujikimu” alihoji.
MWISHO
Comments
Post a Comment