Senyamule awasisitiza wanufaika wa TASAF kutumia pesa kujiletea maendeleo
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wanufaika wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutumia vizuri pesa wanayopewa na mfuko huo katika
kufanyia shughuli mbalimbali za kuingiza kipato ili kujikwamua kiuchumi na
kuondokana na dhana ya kuwa tegemezi katika jamii na taifa kwa ujumla.
Aliyasema
hayo wakati akiwa kwenye ziara fupi ya kutembelea wanufaika wa Mfuko wa TASAF
katika mtaa wa Mchemwa, Kata ya Makutupora, jijini Dodoma iliyokwenda na
Kaulimbiu isemayo ‘TASAF, kwa pamoja tuondoe umaskini’.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, alisema kuwa miongoni mwa malengo ya TASAF ni kuhakikisha
wanajamii wenye kipato cha chini wanainuka kiuchumi na kuwa na kipato cha juu
ili kusaidia kuinua vipato vyao na familia zao kwa ujumla. “Mfuko wa TASAF
umekuja ili kuwafanya wale wenye kipato cha chini kuongezeka na kuanza kupata
kipato cha juu” alisema Senyamule.
Katika
hatua nyingine, aliwahimiza wanufaika wa mfuko huo kuipa thamani pesa hiyo kwa
kufanyia shughuli za maendeleo kwasababu malengo ya TASAF hayawezi kutimia
ikiwa walengwa hawatakuwa na utayari wa kufanikisha dhamira hiyo. “Dhamira hii
haiwezi kutimia ikiwa mlengwa hajataka kuitimiza kwasababu leo tunaweza kusema
tugawe laki moja kwa kila mtu lakini yule mwenye dhamira tutakuta pesa hiyo
imeongezeka na imekuwa laki mbili” alisema Senyamule.
Kwa
upande wake, Mratibu wa TASAF ngazi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sekunda
Kasese alifafanua kuwa katika Mtaa wa Mchemwa kuna kaya 25 zenye wanufaika wa mfuko
huo ambao wanapokea pesa hizo kwa njia ya benki na wengine hupokea pesa
taslimu.
Nae,
mkazi wa Mtaa wa Mchemwa ambae ni mnufaika wa TASAF, Esther Chitojo, mwenye
umri wa miaka 68, aliushukuru mfuko huo kwa kuwawezesha na kuwasaidia kuinua
vipato vyao kwasababu wameweza kupiga hatua moja kwenda hatua nyingine
kimaendeleo. “Nimeshukuru kuletwa kwa TASAF kwasababu imeweza kutuinua sana na
maisha yetu yanaenda vizuri” alisema Chitojo.
Sambamba
na hayo, alieleza kuwa kupitia pesa anazopata kutoka TASAF aliweza kununua
mbuzi wawili walioweza kuzaliana na kufikia mbuzi 12 na baadae alibadirisha
mbuzi hao na kupata ng'ombe jike wawili ambao hadi sasa wamezaliana na kufikia
ng'ombe 12 wanaotoa maziwa ya kuuza na kumfanya aweze kujipatia Kipato.
Mbali
zaidi, alisema kuwa aliweza kuanzisha kilimo cha zao la Choya ambapo baada ya
mavuno hupeleka sokoni kuuza na kupitia fedha hizo alifanikiwa kujenga nyumba
yenye vyumba vitatu na sebule moja. “Kupitia fedha ninazopata kutoka TASAF
nilianzisha kilimo cha Choya na huwa ninauza pamoja na maziwa. Kwahiyo, kwa
kuweka pesa kidogo kidogo nilianza kununua simenti, nikafyatua tofali lakini
mwaka jana niliuza ng'ombe wawili nikanunua mbao na mabati na nilifanikiwa
kujenga nyumba yenye vyumba vitatu na sebule” alisema Chitojo.
Malengo
ya mfuko wa TASAF ni kuzinusuru kaya maskini zaidi kwa kuongeza vipato na fursa
za kujikimu, kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii, kuimarisha lishe bora,
kuongeza mahudhurio ya watoto shuleni, na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za
afya.
MWISHO
Comments
Post a Comment