Vilabu vya michezo vyashiriki mazoezi ya viungo vya mwili jijini Dodoma
Na. Aisha Ibrahim, Mailimbili-DODOMA
Vilabu mbalimbali vya michezo jijini Dodoma,
vimejitokeza kwa wingi katika Bonanza la “Dodoma Aerobics Festival” msimu wa
kwanza, lililofanyika katika kiwanja cha Chinangali Park, kuanzia saa 12:00
asubuhi mpaka saa 6:00 mchana kwa lengo la
kuwakutanisha wanamichezo wote kushiriki mazoezi mbalimbali ya
kuimarisha viungo vya mwili.
Bonanza hilo liliandaliwa na kikundi cha
wakufunzi wa michezo kutoka Jiji la Dodoma 'Dodoma Trainers Group' lilijumuisha
mchezo wa kunyanyua uzito, kupasha mwili, kurukaruka na vikundi vya kukimbia.
Akizungumza wakati wa bonanza hilo, mgeni
rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, aliwasisitiza
wana Dodoma kuendelea kufanya mazoezi kila siku hasa siku ya Jumamosi kama
ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
alivyosisitiza kila mtanzania kujitengea siku ya kufanya mazoezi kwa lengo la
kuimarisha viungo vya mwili. “Mazoezi ni afya, mazoezi ni tiba hivyo,
nawapongeza sana waandaaji wa “Dodoma Aerobics Festival” kwa kuja na hiki kitu
muhimu Jiji la Dodoma na kutambua umuhimu wa michezo” alisema Alhaj Shekimweri.
Aliongeza kuwa, ushiriki wa mazoezi mbalimbali
huleta fursa ya watu kutoka maeneo tofauti kukutana na kujumuika kwa pamoja
katika kuburudika na kubadilishana uwezo na uwelewa wa mambo mbalimbali
yanayohusiana na michezo. "Mazoezi yana tafsiri nyingi na nikisema hivi
najua wana mazoezi wananielewa kwasababu kijamii kujichanganya huleta fursa ya
kukutana na marafiki na viongozi mbalimbali kuburudika nao na kubadilishana
mawazo na uelewa wa masuala ya kimichezo” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa “Dodoma
Aerobics Festival” Emmanuel Juma, alisema kuwa wanajivunia kuanzishwa kwa
tamasha kubwa la kuwakutanisha wana mazoezi kutoka vilabu mbalimbali na kupata
fursa ya kujumuika kwa pamoja kufanya mazoezi ya kuimarisha viungo vya mwili. “Hili
ni tamasha ambalo limekusanya vilabu vyote vya 'jogging' na wafanya mazoezi
kutoka vituo mbalimbali Jiji la Dodoma lakini pia wapo wengine wametoka Wilaya
ya Bahi, Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Tabora na mikoa tofauti tofauti. Hivyo,
nijivunie kuwa hili ni tamasha kubwa na la Kipekee hapa jijini Dodoma” alisema
Juma.
Nae, mwalimu kutoka kituo cha kufanyia
mazoezi “Home Fitness Center” kilichopo Kata ya Nzuguni, Ally Lwambo,
alifafanua kuwa kila mtu ana wajibu wa kufanya mazoezi ya viungo vya mwili kila
siku bila kuzingatia suala la unene au wembamba wa mwili ili kujenga ukakamavu
na uwezo mzuri wa kufikiria. “Ni wajibu wa kila mtu kufanya mazoezi kwasababu
mazoezi ni afya na hayana mwembamba wala mnene hivyo ukipata muda wowote wa
kufanya mazoezi basi shiriki ipasavyo” alisema Lwambo.
Sambamba na hayo, mmoja kati ya washiriki wa
mazoezi hayo Acxa Madinda, alishauri kuwa
mazoezi hayo yasiishie kwa watu wazima badala yake hata watoto waandaliwe
matamasha mbalimbali ya michezo ya kuimarisha viungo vya mwili kwasababu
michezo ni kujifunza na kuburudika. “Kama mnavyoona mimi nilikuja na mtoto
wangu na baada ya kufanya mazoezi amefurahi sana hivyo nìshauri haya matamasha
yasiishie tu kwa watu wazima bali yaandaliwe hata kwa watoto ili nao waweze
kuburudika” alisema Madinda.
Kufanya mazoezi ya mwili kuna faida nyingi
muhimu kwa afya ya mtu kama vile husaidia kudhibiti uzito wa mwili, kusaidia
kuondoa mafuta yasiyohitajika mwilini, kuimarisha misuli na mishipa husaidia
kuboresha hali ya akili na kufikiri.
MWISHO.
Comments
Post a Comment