Dodoma Jiji FC, Gari Limewaka
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imeichakaza Klabu
ya Soka ya Fountain Gate FC, kwa kuichapa bao Moja kwa nunge katika mchezo wa Ligi
kuu ya NBC Tanzania bara, mchezo uliopigwa katika dimba la Jamhuri hapo jana,
bao pekee la Dodoma Jiji FC, liliwekwa kimiani na mchezaji Idd Kipagwile, kwa
mkwaju wa penati mnamo dakika ya 37 ya mchezo.
Baada ya mchezo kutamatika Kocha Mkuu wa
Dodoma Jiji FC, Mecky Mexime alisema “niwapongeze wachezaji wangu kwa kupambana
na kuhakikisha tunashida mchezo. Mchezo ulikua ni mgumu ukizingatia hatuna
idadi ya wachezaji wengi wenye utimamu kimwili lakini wachezaji waliopo kwa
uchache wao wameweza kuonesha umuhimu wao kwenye timu wamepambana kadri ya
uwezo wao tumeweza kushinda mchezo, tumetengeneza nafasi kwa idadi kubwa sana
kipindi cha pili lakini kutokana na presha ya mchezo tukashindwa kuzitumia
lakini kwenye mchezo ujao tutajiandaa kwenda kuhakikisha tunatumia nafasi
tunazotengeneza kwa usahihi”.
Akiongelea malengo ya timu alisema kuwa ni
kukusanya alama kwa kila mchezo ulio mbele yao. “Ili kujiweka katika nafasi
nzuri zaidi mwishoni mwa msimu, na ushindi huu mfululizo kwa mechi za nyumbani
unatuongezea nguvu zaidi ya kupambana huku tukusubiri majeruhi wapone haraka
warudi kwenye timu ili tuje tupambanie malengo yetu kwa pamoja” aliongeza
Mexime.
Nae, nyota wa mchezo huo Mwanakibuta David
baada ya dakika 90 kutamatika aliwashukuru wachezaji wenzake kwa kupambana
kuhakikisha timu inapata matokeo chanya licha ya kukumbwa na wimbi la majeraha
kwa baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu mchezo umeisha
salama na tumeweza kupata alama tatu muhimu, lakini kwa ukubwa niwapongeze
wachezaji wenzangu kwa kupambana kwa dakika zote mpaka tumefanikiwa kushinda
mchezo wa pili mfululizo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipo washukuru mashabiki
wetu ambao wamejitokeza kwa wingi kutuunga mkono, kama wachezaji tumefarijika
sana na tutaendelea kujituma kuhakikisha mashabiki wanafurahi na timu inazidi
kukusanya alama na kupanda katika nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi” alisema
Kibuta.
Katika michezo mitatu ya mwisho Dodoma Jiji
FC, imefanikiwa kukusanya alama saba kibindoni, ikitoa sale mchezo mmoja, ikishinda
michezo miwili. Mchezo ujao Dodoma Jiji FC, itasafiri kuwafuata Nyuki wa
Tabora, Tabora United mchezo unaotarajiwa kuchezwa katika dimba la Ali Hassan
Mwinyi Februari 28 saa 10:00 jioni.
Comments
Post a Comment