Wafanyabiashara kuboresha huduma na kukuza biashara Mwaka 2025
Na. Halima Majid na Shahanazi Subeti, DODOMA
Wafanyabiashara waweka wazi malengo ya
kuboresha huduma ya kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi ya
Jiji la Dodoma mwaka 2025.
Hayo yalisemwa na wafanyabiashara wa eneo
la One Way lililopo katikati ya Jiji la Dodoma wakati wa mahojiano na waandishi
wa habari walipokuwa wanaelezea salamu za jinsi walivyoupokea mwaka mpya 2025.
Mfanyabiashara wa urembo, Luqman Olomi, katika
Mtaa wa One Way alisema changamoto kubwa ni matatizo ya kifamilia yanayopelekea
kurudishwa nyuma kiuchumi na kusababisha biashara yake kuyumba kwa kiasi flani.
"Kuna changamoto za kifamilia zaidi ambazo huwa zinaturudisha nyuma kwa
kiasi kikubwa kwa sababu inabidi utumie mpaka kiasi ambacho umeweka kwa ajili
ya biashara na ili tufanikiwe inatakiwa tujitegemee na tusitegemee cha mtu. Hiyo
ndio siri ya mafanikio na kwa anayoyafanya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan kwa kushirikiana na mashirika mengi na taasisi mbalimbali anafanya
vizuri” alisema Olomi.
Nae Mfanyabiashara wa vitambaa, Barke Boda,
alisema kuwa ana malengo ya kutafuta riziki yake na malengo makubwa ni
kuendelea kutoka sehemu aliyopo kwasasa na kuikuza. “Mwaka huu nina malengo
makubwa naomba Mungu anisimamie katika hilo.
Kwa maana mwaka uliopita haukuwa mzuri kibiashara lakini tunamshukuru sana
tunaendelea vizuri tunatakiwa tusikate tamaa tujipange vizuri ili tuweze
kufikia malengo” alisema Boda.
Mfanyabiashara wa viatu na mabegi, Mwanahamisi
Hamadi, alisema mwaka ameupokea vizuri na anamalengo ya kuendeleza biashara kwa
kuongeza bidhaa zaidi na amesisitiza kuwa makini katika biashara ili kuepuka
matapeli. “Licha ya changamoto nilizozipitia lakini pia nimesema kuwa nina malengo
makubwa mwaka huu kwasababu naamini
utakuwa ni mwaka wa utulivu na ulinzi wa kutosha ili niweze kufanya biashara
zangu kwa amani licha ya kuwa ni mwaka wa uchaguzi” alisema Hamadi.
Mwaka
2025 unatarajiwa kuwa kipindi cha mageuzi makubwa kwa wafanyabiashara wa One Way
huku wakiwa na matumaini ya kuimarisha uchumi wa familia zao na Jiji la Dodoma
kwa ujumla.
MWISHO
Comments
Post a Comment