Viongozi Jukwaa la Wanawake Jiji la Dodoma wawezeshwa mafunzo
Na. Coletha Charles, DODOMA
Viongozi wa Jukwaa la Wanawake Halmashauri ya Jiji la Dodoma
wamewezeshwa mafunzo ya fursa za kiuchumi katika shughuli za biashara, kilimo,
upatikanaji wa mitaji, sheria, ujasiriamali, matumizi ya teknolojia na mikopo
ya asilimia kumi.
Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari
Dodoma kwa lengo la kuwakutanisha wananawake ili waweze kujadili fursa na
changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa shughuli za
kiuchumi.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hidaya Mizega, aliwataka wanajukwaa hao kufahamu
majukumu yao na sheria katika kuwezesha mafunzo kwa wanawake wengi kwa kufahamu
masuala ya uchumi.
Alisema kuwa, viongozi hao wanajukumu katika mitaa na kata
zao kuhamasisha shughuli za kiuchumi kwa kuibua miradi mikubwa na mizuri
kupitia mikopo ya asilimia kumi ili kukuza ongezeko la uchumi kwa wanawake, kwa
kufuata mwongozo mpya ambao umeboreshwa. “Wajumbe wa majukwaa ya uwezeshaji wa
wanawake kiuchumi ngazi ya kata ni wale wanavikundi waliopo katika mtaa husika.
Kwa mwongozo huu kama mwanamke hayupo kwenye kikundi basi huyo siyo mjumbe
wetu. Lakini pia majukwaa haya tumeona kuna changamoto ya nauli na watu kutoka
mbali. Hivyo, serikali ikasema hapana kwa maana hiyo vikao hivi vya jukwaa
vimetiwa nguvu vifanyike katika ngazi za mitaa. Hivyo, basi, kazi ya kata na halmashauri
ni kuratibu” alisema Mizega.
Aliongeza kwa kusema kuwa, kuchelewa kwa mikopo ya asilimia
kumi ni kutokana wa mfumo wa benki kutokukamilika na kwa sababu Dodoma Jiji ipo
kwenye utaratibu wa kutoa mikopo kwa majaribio kupita mfumo huo.
Nae, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Nkuhungu,
Ashura Kimwaga, alisema kuwa, majukwaa hayo yanatakiwa kupewa nguvu katika
kuwahamasisha wanawake kuibua miradi na kuweza kupata mikopo ya asilimia kumi
kwa uharaka zaidi. “Tumekuwa tukiwasumbua sana maafisa maendeleo wa kata na
bila kupata taarifa sahihi lakini leo tumepata majibu sahihi na kipi
kinapelekea kuchelewa kupata mikopo. Hivyo, tumefurahishwa tulikuwa na
kigugumizi lakini tumepewa 'data' kamili. Kwahiyo, tunatakiwa tuvute subira kwa
sababu ina malipo” alisema Kimwaga.
Ikumbukwe kuwa, mafunzo hayo yaliwezeshwa kwenye kata 20 za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment