Kambi: Watoto wenye mahitaji maalum wanahaki ya kusoma
Na. Coletha Charles, CHANG’OMBE
Kata ya Chang’ombe,
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imebainisha na kuwaandikisha watoto wenye
mahitaji maalum kwa lengo la kujiunga na elimu ya awali na msingi kwa mwaka wa
masomo 2025 kwa kushirikiana na wazazi, walezi na walimu.
Afisa Elimu Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Issa Kambi akifanya uchunguzi mwanafunzi mwenye mahitaji maalum
Akizungumza wakati
wa uandikishaji wa watoto hao, Afisa Elimu Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Mwl. Issa Kambi, alisisitiza kuwa jukumu la kuwapatia watoto hao fursa ya
kusoma lipo mikononi mwa wazazi na walezi kwa sababu wanahaki ya kupata elimu
kama watoto wengine kwa kuwajengea msingi bora wa maendeleo.
Alisema kuwa,
serikali imejipanga kuwahudumia watoto wenye mahitaji maluum kwa kuwapokea na
kuwapa mahitaji stahiki na kuhakikisha wanapata nafasi bila kujali changamoto
zao. “Wazazi ukiwa na mtoto usichoke kumlea, ukiona umechoka basi huyo mtoto
amefanikiwa na tusiwakatie tamaa. Watoto wenye umri wa kwenda shule tushirikiane
kuwaleta waje waandikishwe kwenye shule zetu, walimu wapo watawahudumia.
Niwaombe muwaambie na wengine waliobaki nyumbani kuwa, tunapokea watoto wa aina
zote kulingana na mahitaji yao na tunawahudumia” alisisitiza Mwl. Kambi.
Nae, Afisa Elimu,
Kata ya Chang’ombe, Rebecca Haule, alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha
watoto wenye mahitaji maalum wanapata fursa ya kuandikishwa shule kwa ajili ya
kuanza masomo ili waweze kujifunza na kufikia ndoto zao.
Afisa Elimu Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Issa Kambi alifafanua jambo
Alisema kuwa, kila
mzazi mwenye mtoto ambaye ana umri wa kuanza kusoma anapaswa kumuandikisha ili
aanze masomo kwa sababu elimu ni haki yake ya msingi na serikali ya awamu ya
sita imeweka mazingira bora na rafiki ya kujifunza. “Kama kata tumejitahidi
kuhamasisha na wazazi wamejitokeza, tutaendelea kuhamasisha hadi siku ya mwisho
na tunawaomba wazazi na walezi watupe ushirikiano. Tunawaomba wasiache
kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum shule, kwa sababu elimu ni msingi wa
maendeleo ya mtoto na jamii kwa ujumla” alisema Haule.
Kwa upande wake, Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Chang’ombe, Mwl. Bakari Mtembo, alitoa wito kwa wazazi
kutowafungia ndani watoto wenye mahitaji maalum na badala yake kuwapeleka shule
kwa sababu wana haki ya kupata elimu kama watoto wengine.
Alisema kuwa, ubainishaji
wa watoto wenye mahitaji maalum ni hatua muhimu katika kuhakikisha elimu
jumuishi inatekelezwa kikamilifu na ushirikiano unahitajika ili kuhakikisha
watoto hao wanapata msaada wanaohitaji kufikia ndoto zao. “Mwitikio wa wazazi kuwaleta
watoto kuandikishwa kwa ajili ya masomo 2025 umekuwa mkubwa, japo wamefika kwa
kuchelewa huenda hawakupata taarifa ya uandikishaji mapema kutoka kwa viongozi
wao wa mitaa. Lakini pia shule yetu inapokea watoto wenye mahitaji maalum. Hivyo,
wazazi wasione aibu kuwaleta watoto shule” alisema Mwl. Mtembo.
Aidha, mkazi wa
Chang’ombe ambaye ni mzazi wa mtoto mwenye mahitaji maalum, Erika Magomba, aliomba
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasaidia wazazi wenye watoto wenye
mahitaji maalum misaada mbalimbali ya mahitaji katika ukuaji wao. “Niwashauri
wazazi wenzangu kutowaficha watoto kwa sababu hawa watoto wengine wanavipaji
mbalimbali kama kushona na ufundi. Kwahiyo, tujitahidi tuwatoe watoto nje ili
watu wawaone waweze kuwasaidia. Ninawashukuru sana watoto wetu wamepata msaada mkubwa
wa kwenda shule” alisema Magombe.
Katika harakati za
kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata haki zao za msingi ya kupata
elimu, umuhimu wa kubainisha changamoto zao mapema hauwezi kupuuzwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment