Watanzania watakiwa kupambana na rushwa na dawa za kulevya

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

WATANZANIA wametakiwa kushikamana na kupambana na rushwa, dawa za kulevya na uvunjifu wa haki za binadamu ili kujenga jamii iliyo bora.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Simbachawene

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Simbachawene alipokuwa akifungua mashindano ya mdahalo kwa shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kuhusu madhara ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, haki za binadamu na utawala bora katika ukumbi wa St. Gaspar Kisasa jijini Dodoma.

Waziri Simbachawene alisema “baada ya watu kuwa wanashiba, elimu wanatapa kila kitu kinaenda vizuri, wanatazama televisheni wamepata ‘exposure’ mambo ni mazuri wameibuka maadui wengine. Maadui hao ni rushwa, dawa za kulevya na uvunjifu wa maadili na haki za binadamu, hao maadui watatu ni maadui wabaya sana, ni wajibu wa kila mmoja tushirikiane kupambana na maadui hao watatu wapya. Wale maadui watatu wa zamani ujinga, maradhi na umasikini tumewashughulikia vizuri kwa awamu zetu sita za uongozi wa nchi hii. Chembechembe ndogo zilizobaki tuendelee kuzishughulikia lakini sasa tuhamie kwenye maadui hawa watatu rushwa, dawa za kulevya na maadili haki za binadamu na utawala bora”.

Alisema kuwa vijana ndiyo wahanga wakubwa wa maadui hao watatu. “Ninapojikuta nimekaribishwa katika mdahalo huu unaohusisha vijana wa shule za msingi, sekondari na vyuo ninafahamu ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo vya rushwa na dawa za kulevya. Ninafahamu ukitaka kupenyeza uzalendo na kutengeneza watumishi bora wa kesho lazima tuanze na vijana. Mheshimiwa Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na muasisi wa jambo hili na kwamba umeweza kuendeleza maadhimisho haya yakiwa yanafanyika kila mwaka. Mwenyezi Mungu akutie moyo na akubariki sana ili uendeleze juhudi zako hizi njema kwa vijana wa taifa letu” alisema Waziri Simbachawene.

Aidha, alisema kuwa ni vizuri midahalo hiyo ikawa inafanyika nchi nzima ili kuamsha ari ya uzalendo na kuwajengea uwezo wa kujiamini vijana. “Jambo hili linaendelea kuleta mwangwi kwa wengine wengi siyo tu kwenye mkoa kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa vile yeye anazungumzia mkoa wake, lakini mimi kwa nafasi yangu niseme kama lingeenda mikoa yote ingekuwa nzuri zaidi” alisema Waziri Simbachawene.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alitoa pongezi kwa serikali kuelekea kutimiza miaka 60 ya Muungano. “Niwapongeze sana viongozi walioanzisha Muungano na waliouendeleza. Lakini kwa sasa nimpongeze Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar wao wameendelea kuuimarisha Muungano” alisema Senyamule.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule


Vilevile, alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kwa kulipa nguvu suala ya mapambano dhidi ya rushwa na kuonesha dhamira chanya. “Alipoanza mdahalo wa kwanza nilikuwepo ila muitikio ulikuwa mdogo ila mwaka jana muitikio uliongezeka na mwaka huu umeendelea kuimarika kama Muungano wa Tanzania, hongera sana. Mheshimiwa mkuu wa wilaya ameona asilalamike ila ameamua kuchukua hatua, lakini nimpongeze si kwamba anachukua hatua kwa mdomo hata yeye mwenyewe anachukua rushwa kwa vitendo” alisema Senyamule.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema kuwa zipo haki za watu ambazo zimekuwa zikipotea kwa sababu ya vitendo vya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya. “Kwa maelekezo ya Rais, tushughulikie kero na tunamshukuru mkuu wa mkoa ametuongoza tumeanzisha kampeni katika mkoa wake ya ‘Kero yako, wajibu wangu’. Tunashiriki vita hii kwa kutoa elimu kujenga kizazi ambacho kesho kitachukia uharibifu wa maadili katika nchi yetu, watachukia matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wanajua madhara yake na watachukia rushwa, sisi samaki tunamkunja angali mbichi. Wanafunzi hawa wakielewa nyuma yao ni wazazi, nyuma yao ni marafiki lakini wao pia baadhi yao ni viranja wanaongea na wenzao, wanawadogo zao naimani taarifa hizi zitafika kwa watu wengi” alisema Shekimweri.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri 


Kwa upande wa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Dodoma, John Joseph alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa klabu za kupinga rushwa ni kuwajengea moyo wa uzalendo na uadilifu na kuongeza uelewa juu ya ubaya wa rushwa kwa wanafunzi. “Uanzishwaji wa klabu hizo ulitokana na Takukuru kuamini kwamba vijana katika taifa ni rasilimali muhimu na chimbuko la mabadiliko. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa kuwarithisha maarifa, uadilifu na moyo wa uzalendo. Mkoa wa Dodoma tuna jumla ya klabu za wapinga rushwa 1,081 kwa shule za msingi, sekondari na vyuo” alisema Joseph.



Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Dodoma, John Joseph




MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma