Miaka 63 ya Uhuru, watanzania waaswa kutunza na kuthamini Uhuru
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Watanzania
wameaswa kutunza na kuthamini uhuru kwa kufanya mambo yanayoleta amani na
usalama wa nchi, ili kufurahia matunda ya uhuru yaliyopatikana ndani ya miaka
63 tangu tarehe 09 Desemba, 1961.
Hayo,
yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokuwa akizungumza
na mamia ya wananchi waliohudhuria katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka
63 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika makutano ya Barabara ya Mzunguko
(Ring Road) katika Kata ya Makutupora, jijini Dodoma.
Senyamule
alisema “ili
uhuru huu tuendelee kuufurahia na kuuenzi, kwanza tuhimize amani na usalama wa
nchi yetu kwasababu ni msingi wa mafanikio. Huu uhuru tunausherekea kwasababu
bado tunaulinda, usije ukafikiri ukipata uhuru ndio imeisha, unaweza ukapata
uhuru na baadae ukapotea tena kwasababu unaweza ukaingiliwa. Tuendelee kutunza
kwa kufanya mambo ya amani na utulivu”
Akizungumzia
mafanikio yaliyopatikana katika Miaka 63 ya Uhuru, aligusia
mafanikio mbalimbali katika miundombinu na fursa zilizopo nchini ukilinganisha
na miaka ya nyuma ambayo Tanzania Bara ilikuwa haijajipatia uhuru wake. “Ndugu
zangu tunapoongelea Miaka
63 ya Uhuru, Mkoa wetu wa Dodoma unaendelea kukua kwa ‘speed ya 5G’ yaani kasi
ya kukua kwa Mji wa Dodoma kila mtu anaishangaa, kuanzia sekta moja kwenda
sekta nyingine. Leo tumesimama kwenye hiyo Barabara ya Mzunguko, barabara hiyo
ya mzunguko haipatikani sehemu nyingine yoyote Tanzania, Afrika Mashariki,
Afrika ya Kati, kwa ukubwa wake, upana wake na urefu wake, inapatikana Dodoma
peke yake” alisema Senyamule.
Akiongelea
kuhusu kaulimbiu ya maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara,
isemayo “Uongozi Madhubuti na
Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo yetu”
alisema Tanzania inabahati kuwa na uongozi madhubuti ambao unafanya kila
jitihada za kimaendeleo sambamba na kushirikisha wananchi katika kila hatua ya
maendeleo ya nchi. “Sisi kama watanzania tunayo bahati kwasababu tumekuwa na
uongozi madhubuti
toka uhuru wa nchi yetu, watu wakianza kumuelezea Baba wa Taifa hawamalizi
kurasa kwa sifa za uongozi wake. Vilevile, tumepata viongozi wazuri kwa kila
awamu. Lakini kaulimbiu hii inaendelea kusema ushirikishwaji wa wananchi ni
msingi wa maendeleo. Katika historia ya nchi yetu tumeshuhudia mambo mengi
lakini kwa wakati huu ninaona ushirikishwaji umepita nyakati nyingine nyingi.
Tunaona jinsi ambavyo Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotamani mambo yote
yanayoamuliwa kwa ajili ya watanzania yatokane na watanzania wenyewe, ndio
maana wakati wote utasikia anasema ninaunda tume, iende kwa wananchi ikapokee
mawazo ili tuje tutengeneze jambo, kwasababu yeye anaamini katika
ushirikishwaji” alisema Senyamule.
Kwa
upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe, aliwaasa wananchi
katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kuwajibika kwa kufanya
kazi ili kuwa huru. “Hatuwezi kujidai tuko huru kama hatufanyi kazi, kwasababu
bila kufanya kazi tutakuwa watumwa, kama sio mtumwa wa jirani, nchi jirani au
nchi nyingine. Kwahiyo, msisitizo wangu mkuu katika hafla hii, uhuru ni kazi,
usipofanya kazi hatutakuwa huru. Uhuru kama taifa unaanzia pale ambapo mtu
mmoja mmoja anapokuwa na uhuru. Kwahiyo, tufanye kazi kama mtu binafsi, lakini
tufanye kazi ili taifa letu liwe huru” alisisitiza Prof. Mwamfupe.
Vilevile,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Prof. Don Santos Silayo, aliwataka
wananchi kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania bara kwa kushiriki katika kupanda
miti ili kutunza ikolojia. “Siku ya leo tunapoadhimisha miaka
63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, nchi yetu inaowajibu wa kulinda
na kudumisha mazingira yetu kwasababu mazingira yetu ndiyo yanayotutunza sisi.
Sisi hatuwezi kuwa salama kama mazingira sio salama. Kwahiyo, tunaowajibu wa
kutunza, kwa dhamana ya leo na jambo tulilolifanya la kupanda miti ni jambo la
kushukuru kwamba kila mmoja anapata nafasi ya kuona umuhimu wa kushiriki kwenye
uumbaji” alisema Prof. Silayo.
Maadhimisho
ya Miaka
63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, jijini Dodoma yalianza na zoezi
la upandaji miti katika eneo la barabara ya pete "ring
road"
katika eneo la Barabara ya Nala- Makutupora. Takribani
miti 100,000 itapandwa kuzunguka eneo hilo, ambapo mashimo mia nane yamechimbwa
na miti 800 ilitandwa, awali ilipandwa miti 850. Miti hiyo imepandwa kwa lengo
la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani ili kukabiliana na mabadiliko
ya tabia ya nchi yanayoikumba Dunia kwa sasa.
MWISHO
Comments
Post a Comment