Bonanza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali jijini Dodoma 2024 lafana
Na. John Masanja, DODOMA
Mwakilishi wa
Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Neema Kilongola ambaye ni Afisa Michezo
wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ameshiriki katika Bonanza la kufunga mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Dodoma.
Aidha, bonanza hilo lenye kaulimbiu isemayo "Mazoezi
ni Tiba" limefanyika katika uwanja
wa michezo wa Shule ya Sekondari Jamhuri na kuhudhuriwa na wanamichezo na
wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza na wanamichezo hao, Kilongola alisema kuwa matokeo yanayotegemewa kutokana na bonanza hilo ni ongezeko la aina ya michezo na ushiriki wa jamii katika michezo, ongezeko la uelewa wa jamii na mabadiliko ya tabia juu ya ufanyaji wa mazoezi pamoja na ushuhuda wa watu juu ya kupungua kwa maumivu ya mwili na uzito.
Alitoa rai kwa mashirikia yasiyo ya kiserikali kuanzisha uchangiaji wa jamii na wadau ili kuwapa motisha walimu na wataalamu wa afya na manunuzi ya vifaa vya michezo.
"Niwashauri kuingiza ratiba ya michezo katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na ya serikali kwenye eneo la Halmashauri husika" alisema Kilongola.
Kwa upande wake Carle Silus Lyimo, Mwenyekiti wa kikosi kazi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali alisema "lengo kuu ni kuanzisha michezo endelevu ngazi ya jamii kwa vijana, watu wazima, na wazee kwa kuzingatia jinsia ili kuongeza mabadiliko ya tabia ya kufanya mazoezi na kupunguza madhara ya magonjwa yasiyoambukizwa".
MWISHO
Comments
Post a Comment