Wananchi Chikole wahamasishwa kupiga kura Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Na. Dennis Gondwe, MSALATO
Wananchi wa Mtaa wa Chikole wamehamasishwa kujitokeza
kushiriki zoezi la kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 katika Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa ili waweze kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika maendeleo.
Patrick Sebyiga (wa kwanza kushoto) akihamasisha baadhi wa wakazi wa Mtaa wa Chikole
Hamasa hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu ya hamasa ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alipoongoza timu hiyo kutoa
hamasa kwa wananchi wa Mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato kujitokeza siku ya
kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Sebyiga ambae pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma anaeratibu Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa alisema kuwa
wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. “Mtakumbuka
tumemaliza zoezi la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, kazi iliyobaki
ni kujitokeza siku ya kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024. Mjitokeze kuchagua
viongozi wenye sifa, watakaoshirikiana nanyi katika kuleta maendeleo. Mchague
kiongozi bora si bora kiongozi” aliongea Sebyiga kwa msisitizo.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeunda timu sita
mahususi kwa ajili ya kuhamasisha umma kushiriki zoezi la kupiga kura katika Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024 chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali
za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
MWISHO
Comments
Post a Comment