Wajasiriamali wanufaika na Nishati Jadidifu Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wajasiriamali
kutoka kata za pembezoni za Hombolo Makulu, Ipala, Mbalawala, Chihanga na
Mnadani katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamenufaika na mradi wa nishati
jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji uliolenga kuimarisha na kuboresha miradi ya
wajasiriamali wa pembezoni.
Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Santiel Mmbaga
Hayo
yalisemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma,
Santiel Mmbaga wakati wa mkutano na wadau mbalimbali wenye lengo mahususi la
utoaji taarifa ya utekelezaji wa mradi wa matumizi ya nishaji jadidifu kwa
matumizi ya uzalishaji kwa mwaka 2022 hadi 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya
Mkoa wa Dodoma.
Mmbaga
alisema “halmashauri imeweza kunufaika sana na miradi hii ya Kakute ambayo imetufungia
nishati hii jadilifu kwenye maeneo ya pembezoni, kwasababu wananchi wetu
walikuwa wanahitaji huduma, walikuwa wanafanya kilimo, walikuwa wanachajisha
simu lakini sio kwa kiwango hicho. Lakini saizi kilimo kilichokuwa kinafanyika
kwa udogo sasa hivi kinafanyika kwa ukubwa zaidi kwasababu ya nishati ambayo Shirika
la Kakute limeweza kuwafungia wananchi wetu. Kwahiyo, kama halmashauri tunaona
wananchi wetu wameweza kuongeza kipato kutoka hali ya chini kwenda ya juu
kidogo kulingana na hii nishati jadidifu. Kwahiyo, tunaendelea kuwashukuru sana
na kuwakarisbisha ili tuendelee kufanya kazi kwa ushirikiano”.
Akizungumzia
maendeleo ya wananchi katika jamii, aliishukuru serikali na Shirika la Kakute
Projects kwa uwezeshaji walioufanya katika kata hizo kwasababu mradi umesaidia
kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. “Tunashukuru sana
kwasababu wananchi wetu wameweza kupata maendeleo, wengine wameweza kupeleka
watoto shule, wengine walikuwa hawana umeme wameweza kupata umeme ina maana
watoto watasoma, watafaulu vizuri. Kwahiyo, tunaendelea kutoa shukrani zetu kwa
serikali na Shirika la Kakute Projects, tuendelee kushirikiana ili tuweze
kuinua wananchi wetu” alisema Mmbaga.
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Mbalawala, Hessein Karume
aliipongeza serikali kwa kuruhusu wadau mbalimbali kuunga mkono harakati za
maendeleo ya jamii na kueleza namna ambavyo Kata ya Mbalawala imenufaika na
mradi wa nishati jadidifu kwa ajili ya uzalishaji. “Shirika hili la Kakute Projects
katika Kata ya Mbalawala, limewezesha wajasiriamali watatu na wajasiriamali hao
wameleta mchango mkubwa sana katika Kata ya Mbalawala. Kwa mfano kuna sehemu ya
kuchajishia simu, kuna uzalishaji wa kuku na kutotolesha kuku, hii yote ni
miradi iliyowezeshwa na Kakute Projects. Pia watu wa Mbalawala wameweza kuwa na
sehemu ya kukutana pamoja kwa mfano, mmoja wa wajasiriamali ana kituo cha
kuonesha mpira na kuchajisha simu, na kimsingi tunaweza kusema kwamba, tumepata
maendeleo makubwa ya kuonekana kupitia wajasiriamali hao. Kwahiyo, naipongeza
serikali kwa kuwaruhusu wadau kama hawa kuweza kuja na kuunga mkono harakati za
maendeleo” alisema Karume.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DOM
Energy Solutions and Designing Ltd, Anthony Machai, ambae ni msambazaji wa teknolojia
katika mradi huu alipongeza juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya kutokomeza
matumizi ya nishati chafu na hivyo kumuunga mkono katika kusambaza teknolojia
ambayo ni rahisi kwa wajasiriamali wa baadhi ya kata zilizopo jijini Dodoma kwa
kushirikiana na Kakute Projects. “Tunajishughulisha na ufungaji wa mitambo ‘solar’
mbalimbali katika Jiji la Dodoma na Tanzania nzima. Ukiangalia kwa sasa hivi
pia rais wetu yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha wananchi kwa asilimia kubwa
tunatumia nishati safi ambayo inatunza mazingira. Na sisi kama wadau wa
nishati, tunampongeza kwa jitihada nyingi sana anazozifanya kutafuta wafadhili
wengi watakaoiwezesha jamii yetu kupata nishati hii ambayo ni rahisi na kila
mmoja anaweza akamudu” alisema Machai.
Kwa
upande wake mjasiriamali Lucas Japhet, aliipongeza serikali kwa kuwaletea wadau
ambao wamekuwa ni chachu kubwa sana katika kukuza biasahara zao na kuyafikia
malengo kwa teknolojia nzuri walizowekewa. “Nimefungiwa mtambo wa ‘solar’
na umenirahisishia mimi kufanyakazi zangu kwa uhuru zaidi na kwa wepesi zaidi
na mpaka sasahivi kuna mafanikio mazuri nimeyafikia na kikubwa ninafanya kazi
kwa urahisi zaidi bila shida yoyote. Niishukuru serikali yetu ya Tanzania kwa
kutuletea wadau kama hao wanaotuwezesha sisi wajasiriamali kupata nishati na hata
kwa jamii pia” alisema Japhet.
Mradi
wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji Dodoma ulianzishwa mwaka 2022 na
kuweza kuzifikia kata tano ambazo ni Mbalawala, Chihanga, Hombolo Makulu,
Mnadani pamoja na Ipala na kuwafikia wajasiriamali 15 ambao walipatiwa mitambo
ya kuendesha biashara zao za uzalishaji.
Comments
Post a Comment