Wajasiriamali Jiji la Dodoma wahimizwa kurasimisha biashara zao
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wajasiriamali
katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamehimizwa kurasimisha biashara zao kwa
lengo la kuwa na wigo mkubwa wa kuweza kukopa katika taasisi za kifedha kwa
sababu watakuwa wanatambulika kwa mujibu wa sheria.
Katibu Mtendaji wa Shirika Kakute Projects, Livinus Manyanga akiongea na wadau
Hayo
yalisemwa na Katibu Mtendaji wa Shirika Kakute Projects, Livinus Manyanga
alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mradi wa nishati jadidifu, wadau wa
serikali, viongozi wa sekta ya biashara na wazalishaji wa teknolojia katika
mkutano wa wadau wa mradi wa nishati jadidifu kwa matumizi ya uzalishaji
uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Mkoa uliyopo Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
“Tumejaribu
kufanya kazi kwa karibu sana na vile vikundi ambavyo vimekopeshwa mikopo na
halmashauri tofauti na hii misaada ambayo tumeitoa sisi, inaonesha wazi kwamba
changamoto namba moja ni kwamba, mjasiriamali mdogo mpaka aweze kurasimisha
biashara yake ni hatua ndefu na hawapendi kuchukua hatua ndefu kiasi hicho. Pia
nidhamu ya matumizi ya pesa, kujua hii pesa imetoka wapi na inatakiwa kupelekwa
wapi inakuwa ni ngumu kidogo. Tunazidi kusisitiza, uwekaji wa kumbukumbu,
mpango wa biashara na kurasimisha biashara ni vitu vya msingi sana” alisisitiza
Manyanga.
Akiongelea
suala la teknolojia katika mradi, alisema kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kuwafikia walengwa na imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha biashara zao. “Teknolojia
imetengenezwa vizuri na inaonesha muelekeo wa kuwaongezea uzalishaji na
pia kuboresha maisha yao kwa ujumla” alisema Manyanga.
Kuhusu
suala la wadau wa kifedha, alisema mradi unashirikiana na taasisi mbalimbali za
kifedha ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo katika kata zilizopo Halmashauri
ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuboresha miradi na kuimarisha usambazaji wa
teknolojia. “Mradi unalenga kuwashirikisha wajasiriamali na wadau wa fedha kama
SACCOS, VICOBA pamoja na Benki. Pamoja
na mafunzo tuliyowapatia wajasiriamali waliopo maeneo ya pembezoni, uelewa wao
ni wa taratibu, wanafahamu kila kitu lakini kutekeleza ni taratibu” alisema
Manyanga.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa DOM Energy Solutions and Designing Ltd,
Anthony Machai, ambae ni msambazaji wa teknolojia katika mradi huu alipongeza
juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, katika kampeni ya kutokomeza matumizi ya nishati chafu na hivyo,
kumuunga mkono katika kusambaza teknolojia ambayo ni rahisi kwa wajasiriamali
wa baadhi ya kata zilizopo jijini Dodoma kwa kushirikiana na Kakute Projects.
“Tunajishughulisha
na ufungaji wa mitambo ya ‘solar’ mbalimbali katika Jiji la Dodoma na
Tanzania nzima. Ukiangalia kwa sasahivi pia rais wetu yupo kwenye mchakato wa
kuhakikisha wananchi kwa asilimia kubwa tunatumia nishati safi ambayo inatunza
mazingira. Na sisi kama wadau wa nishati, tunampongeza kwa jitihada nyingi sana
anazozifanya kutafuta wafadhili wengi watakaoiwezesha jamii yetu kupata nishati
hii ambayo ni rahisi na kila mmoja anaweza akamudu” alisema Machai.
Kwa upande wake
mjasiriamali, Lucas Japhet ameipongeza serikali kwa kuwaletea wadau ambao
wamekuwa ni chachu kubwa sana katika kukuza biasahara zao na kuyafikia malengo
kwa teknolojia nzuri walizowekewa. “Nimefungiwa mtambo wa ‘solar’ na
umenirahisishia mimi kufanyakazi zangu kwa uhuru zaidi na kwa wepesi zaidi na
mpaka sasahivi kuna mafanikio mazuri nimeyafikia na kikubwa ninafanya kazi kwa
urahisi zaidi bila shida yoyote. Niishukuru serikali yetu ya Tanzania kwa kutuletea
wadau kama hawa wanaotuwezesha sisi wajasiriamali kupata nishati na hata kwa
jamii pia” alisema Japhet.
Mradi wa nishati jadidifu
kwa matumizi ya uzalishaji Dodoma ulianzishwa mwaka 2022 na kuweza kuzifikia
kata tano ambazo ni Mbalawala, Chihanga, Hombolo Makulu, Mnadani pamoja na
Ipala na kuwafikia wajasiriamali 15 ambao walipatiwa mitambo ya kuendesha
biashara zao za uzalishaji. Pia ulilenga kuimarisha na kuboresha miradi ya
wajasiriamali wa pembezoni iwe na tija zaidi kwa kuunda ushirikiano kati ya
wasambazaji wa suluhisho za teknolojia ya nishati jadidifu na kujenga msingi wa
maendeleo endelevu kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ngazi ya kata na
wadau wengine wa maendeleo.
MWISHO
Comments
Post a Comment