Taasisi zatakiwa kupanda miti kukijanisha Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Taasisi
zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na wananchi, wamehimizwa kupanda
miti katika maeneo wanayofanyia kazi na wanayoishi ili kuifanya Dodoma iwe ya kijani
na kukabiliana na madiliko ya tabia ya nchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya akipanda mti
Hayo
yalisemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya alipokuwa akizungumza
na wadau mbalimbali katika zoezi la upandaji miti kwa awamu ya pili lililohusu wazaliwa
wa mwezi Novemba lililofanyika tarehe 18 Novemba, 2024 katika eneo la Jakaya
Kikwete Square, Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Tumeshaanza
kuyagundua maeneo kama matatu hivi, lakini hili ni la pili tutatekeleza Januari
au Februari, tayari tumeshaongea na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na
watatupatia. Maeneo katika Jiji la Dodoma yapo, Dodoma kuwa kijani inawezekana.
Watu wanaishi na historia kuwa Dodoma haistawi, ni kavu, ni kame. Hapana, Dodoma
sio kame na mifano ipo, mimi ninawaambieni, tafuteni muda, mzunguke mitaani
muangalie kwenye nyumba za watu, zilizowekewa fensi utakuta ndani kuna miti
kijani kabisa, lakini nje ya fensi hakuna miti ya kijani. Nawapongeza watu wote
wanaofanya hivi kwasababu ilikuwa ni agizo la Jiji la Dodoma, kuna sheria ndogo
iliyoundwa katika kila kibali cha ujenzi unachopewa ni lazima upande miti
isiyopungua mitano ikiwemo miti ya matunda na miti mingine ya vivuli”
Aidha,
aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kuunga mkono kampeni ya ‘Mti wangu, Birthday
yangu’ kwa kusaidia kutoa miti na maji kwa ajili ya kuunga mkono jitihada hiyo
ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kukabiliana na madiliko ya tabia ya nchi. “Naomba
nichukue fursa hii bila kupepesa macho, niwashukuru sana NMB, walipewa jukumu na
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kuwa miti hii waendelee kuitunza, lakini Chuo Kikuu cha
Dodoma ndio wenye eneo hili, nao kila siku wapo hapa wakisaidiana na timu ya
wataalamu wa UDOM na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Ninawashukuru sana kwa malezi
mazuri ambayo miti hii mmeipa, ninawashukuru sana watu wa (TANESCO) hii ni mara
ya pili mnakuja kwa wingi, nawapongeza sana (TARURA) na taasisi zingine zote
zilizofika, naombeni katika ofisi zenu pia mkapande miti. Sio muda wote
tunakuwa kazini wakati mwingine tunapumzika kwahiyo pangeni siku mpande miti na
Taasisi zote zillizopo Dodoma tuhakikishe kwenye ofisi zetu zote tupande miti”
alisisitiza Mmuya.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya akihutubia mamia ya wazaliwa wa mwezi Novemba na wadau wengine wa Mazingira
Akiongelea
kuhusu maendeleo ya upandaji miti katika eneo lililotengwa, kuanzia Oktoba
mpaka sasa Novemba, Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, David Chitemo,
alitoa tathimini kwa ujumla ya zoezi zima.
“Tumezindua
zoezi hili la “Mti wangu, Birthday yangu” mwezi wa kumi, ambayo ilikuwa siku
ya kuzaliwa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, tulianza wa kusafisha eneo ambalo
lina ukubwa wa ekari saba, eneo lote lina ekari kumi, na bado kuna ekari tatu
zinazoendelea kusafishwa. Awamu ya kwanza katika uzinduzi tulipanda mita 780,
iliyiohusisha miti ya matunda na miti mingine ya vivuli, tulipopata wadau
wengine tuliongeza haya mashimo 492 ambayo ndio tumepanda leo. Hiyo, miti
tuliyopanda mwezi wa kumi ni miti saba tu ndio iliyokufa, miti maji miwili,
miembe miwili, mijohoro miwili na mzambarau mmoja. Lakini yote tulisha ‘replace’
kuweka mipya. Changamoto ni maji, tunawashukuru wote kila mmoja kwa jitihada
zake na kwapamoja tutashinda. Leo tumepanda miti 492, kwasasa hakuna shimo
lililobaki bila mti” alisema Chitemo.
Kwa
upande wake Afisa Msaidizi uduma kwa wateja (TANESCO) Dodoma, Regina Mkalawa
alitoa rai kwa watanzania kutunza mazingira kwa kubainisha faida za utunzaji miti
na kutotumia nishati chafu ya kupikia kama kuni na mkaa ikiwa ni juhudi ya
kuunga mkono kampeni ya matumzi ya nishati safi ya kupikia, iliyoanzishwa na
Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Sisi
kama wadau, TANESCO Mkoa wa Dodoma, tumehamasika kwa kiasi kikubwa sana
kwasababu tunajua umuhimu wa upandaji miti na tunajua faida za miti. Miti ni
kichocheo kikubwa cha mvua, tunapokuwa tunaharibu miti yetu au misitu tunachangia
kwa asilimia kubwa kutopata mvua ya kutosha. Na tunapokuwa tunapanda miti kwa
wingi tunajiwekea asilimia kubwa ya mvua kunyesha.
Akizungumzia
suala la nishati safi ya kupikia, aliwataka wananchi kutunza mazingira na
kuacha kukata miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa ambayo hupelekea changamoto
ya kiafya hasa kwa akina mama wanaotumia nishati chafu ya kupikia. “Umuhimu
mkubwa wa kutumia nishati safi ya kupikia kwanza inaturahisishia kazi za jikoni,
mwanamke anaetumia jiko la mkaa yaani nishati chafu na anaetumia nishati safi
ya kupikia tofauti yao katika muda ni kwamba mwanamke anaetumia nishati safi
badala ya kutumia dakika 30 kupika chakula atatumia labda dakika 15 lakini
anaetumia mkaa atatumia karibu lisaa lizima. Kwahiyo, nishati safi imesaidia kurahisisha
muda ambao unaupoteza na utafanya majukumu mengine ya kimaendeleo. Changamoto
ya kutumia nishati chafu ya kupikia inapunguza umri wa kuishi, mama atapuliza
mkaa kwa muda mrefu atapata kifua, atapata magonjwa pia ‘life span’
inapungua, labda tunasema ‘life span’ ya mtanzania kwa sasa ni miaka 45,
sasa baada ya mama kuishi miaka hiyo ataishi labda miaka 30 na yote hii ni
kwasababu ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia” alisisitiza Mkalawa.
Vilevile,
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambae pia ni mdau wa Mazingira na Katibu wa
Klabu ya Mazingira Endelevu (ESCUDOM), Agape Latyandumi aliwataka wananchi
kutunza na kuthamini Mazingira kwa kupanda miti ili kuepukana na majanga ya
asili kutokana na hali ilivyo kwasasa ya mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Niko
hapa kuwaambia wananchi na watanzania kwa ujumla tupende kutunza Mazingira na ‘kusupport’
kampeni hii ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa
yaliyojitokeza kwa sasa. Natoa wito kwa wananchi kuwa kila mtu aliye na mti nyumbani
autunze na kama hana mti inahitajika apande mti katika eneo analoishi ili
kuunga mkono kampeni hii ya upandaji miti katika Mkoa wetu wa Dodoma” alisema Latyandumi.
Kampeni
hii ya ‘Mti wangu, Birthday yangu’ ilizinduliwa rasmi Oktoba 18, 2024 na
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwenye eneo la Jakaya Kikwete Square
ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma, yenye lengo la kuifanya Dodoma iwe ya kijani
ambapo imewakutanisha wadau mbalimbali wa Mazingira, wanafunzi pamoja na
wazaliwa wa mwezi Novemba. Miti 780 ilipandwa kwenye eneo la ekari saba wakati
wa uzinduzi wa kampeni na mwezi Novemba jumla ya miti 492 imepandwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment