Wananchi waliojiorodhesha Mkonze wawe Mabalozi kuhamasisha wengine
Na. Dennis Gondwe, BWAWANI, MKONZE
WANANCHI waliojiorodhesha katika orodha ya wapiga kura
wameshauriwa kuwa mabalozi ili kuhamasisha wenzao ambao hawajajiorodhesha
kufanya hivyo mapema ili kuepuka foleni siku ya mwisho hatua itakayowawezesha
kuchagua viongozi bora.
Mkazi wa Mtaa Bwawani, Kata ya Mkonze, Patrick Richard baada ya kujiandikisha
Rai hiyo ilitolewa na mkazi wa Mtaa Bwawani, Kata ya Mkonze,
Patrick Richard muda mfupi baada ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura
katika kituo cha Ofisi ya Afisa Mtendaji Mtaa wa Bwawani mapema leo.
Richard alisema “mimi nimetumia muda mfupi sana, chini
ya dakika moja kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wakati nilijua
nitatumia muda mrefu. Kumbe hata wakija watu 10 kwa pamoja watatumia chini ya
dakika 10 kujiandikisha. Wito wangu wananchi waje kwa wingi kujiandikisha
katika kituo hiki kilichopo kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Bwawani. Sisi
ambao tumeshajiandikisha na kuona uandikishaji ulivyo tuwe mabalozi tuwashawishi
na wengine ambao hawajajiandikisha kuja kwa sababu hawapotezi muda kabisa”.
Akiongelea lengo la kujiandikisha kwake alisema kuwa pamoja
kuwa ni haki yake ya kikatiba, pia anategemea kugombea nafasi ya uongozi katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “Mfano, mimi natarajia kugombea nafasi ya mjumbe
wa kamati ya mtaa. Hivyo, ninawajibu wa kuhamasisha wananchi wajitokeze kujiandikisha
ili waje kushiriki katika kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”
alisema Richard.
Zoezi la kuandikisha wananchi katika orodha ya wapiga
kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilianza tarehe 11 Oktoba, 2024 likitarajiwa
kukamilika tarehe 20 Oktoba, 2024 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika
tarehe 27 Novemba, 2024.
Mabango ya taarifa muhimu yalimoyandikwa katika Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Bwawani
MWISHO
Comments
Post a Comment