Viongozi bora wanachaguliwa na wananchi waliojiorodhesha
Na. Dennis Gondwe, MWAJA, CHAMWINO
VIONGOZI bora wa serikali za mitaa wanachaguliwa na
wananchi waliojiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili waweze kushiriki Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa.
Mkazi wa Mtaa wa Mwaja, Kata ya Chamwino, Josephine Joseph wakati akijiandikisha katika orodha ya wapiga kura
Kauli hiyo ilitolewa na mkazi wa Mtaa wa Mwaja, Kata
ya Chamwino, Josephine Joseph alipoongea na mwandishi wa habari hii muda mfupi
baada ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika kituo cha Shule ya
Msingi Chinangali.
Joseph alisema kuwa kujiandikisha ni haki yake na haki
ya kila mwananchi mwenye sifa za kujiandikisha. “Viongozi bora wa serikali za
mitaa wanachaguliwa na wananchi wenyewe. Hivyo, ili uweze kumchagua kiongozi
bora, sifa ya kwanza uwe umejiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura katika
mtaa wako. Bahati nzuri sifa ni za kawaida sana, kwamba awe na umri wa kuanzia
miaka 18 na kuendelea, awe mtanzania mwenye akili timamu zaidi awe ni mkazi wa
mtaa ambao uchaguzi unafanyika. Hii ni haki ya kila mtu mwenye sifa
kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa” alisema Joseph.
Akiongelea tofauti ya zoezi lililopita la uboreshaji
wa daftari la kudumu la wapiga kura na orodha ya wapiga kura kwa ajili ya
uchaguzi wa serikali za mitaa alisema kuwa uboreshaji daftari la kudumu la
wapiga kura ulilenga maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Orodha ya wapiga kura itahusu kumchagua mwenyekiti wa mtaa na halmashauri yake.
Zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la mpiga kura ulilenga kuboresha taarifa
za watu waliohama toka sehemu moja kwenda nyingine, kupoteza kitambulisho cha
mpira kura na kuandikisha watu waliofikisha miaka 18 ila orodha ya wapiga kura
inahusisha wananchi wanaoishi katika mtaa husika, aliongeza.
Alisema kuwa viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu
sana katika jamii. “Viongozi hawa ndiyo wanaosaidia katika kuhamisisha shughuli
za maendeleo na shughuli nyingine za kijamii kama usafi wa mazingira na
utunzaji wa mazingira” alisema Joseph.
Mtaa wa Mwaja ni moja kati ya mitaa minne inayounda
Kata ya Chamwino ukiwa na vituo vya kuandikisha wapiga kura vitatu.
MWISHO
Comments
Post a Comment