Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Wafanyabiashara wamo
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wafanyabiashara Halmashauri ya Jiji la
Dodoma wamehamasishwa kujitokeza kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura ili kupata
viongozi walio bora ambao wanatambua wajibu wao ili kuwawezesha wafanyabiashara
kutatua changamoto zao katika biashara.
Meneja wa Hoteli ya Spring Hills, William Mndeme akielezea umuhimu wa wafanyabiashara kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa Hoteli
ya Spring Hills, William Mndeme alipokuwa akiongea na waandishi wa habari
kuhusu umuhimu wa wafanyabiashara kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwa
ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Meneja Mndeme aliwashauri wafanyabiashara
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuitikia wito wa kwenda kujiandikisha ili
waweze kuchagua viongozi walio bora na wenye manufaa katika kukuza uchumi wa
nchi. “Ili tuweze kufanya biashara vizuri, lazima tuwe na viongozi bora na
viongozi wanaotambua wajibu wao, ili kuweza kutusaidia sisi wafanyabiashara
pale tunapokuwa na changamoto. Hivyo, ili kupata viongozi walio bora watakaowezesha
mazingira ya biashara kuwa mazuri wafanyabiashara wanawajibu wa kujiandikisha
kwenye orodha ya wapiga kura ili washiriki katika uchaguzi wa viongozi wa
serikali za mitaa” alisema Mndeme.
Aidha, aliipongeza Kamati ya Usimamizi
wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa hamasa ambazo zinaendelea huko mitaani kwa
lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika orodha ya wapiga
kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba,
2024. “Zoezi la kujiandikisha linakwenda vizuri, lakini pia kila ninapopita
ninaona mabango au kukutana na matangazo ya uchaguzi wa serikali za mitaa. Kwahiyo,
linakwenda vizuri sijaona changamoto yeyote, ni zoezi ninaloona limeanza vizuri
na linaenda vizuri, watu wanajiandikisha” alisema Mndeme.
Pia, alitoa rai kwa wafanyabiashara na wananchi
wote kujitokeza kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura kabla zoezi
halifungwa. “Ninawaomba wafanyabiashara wenzangu waitikie hili kwa moyo wao
mmoja kwasababu itakuwa ni faida kwetu, ningewaomba mpaka hiyo tarehe 20 wawe tayari
wamejiandikisha ili tuweze kuchagua viongozi watakaotusikiliza maoni yetu. Pia
ni haki ya kila mtanzania kujiandikisha, mtu aliyefikisha umri wa kupiga kura,
mika 18 na kuendelea na uwe mkazi wa eneo husika, uwe raia wa Tanzania na uwe
na akili timamu. Na mtu atakae jiandikisha katika eneo zaidi ya moja atakuwa
amepoteza sifa za kuwa mpiga kura” alisema Mndeme.
Zoezi
la kuandikisha wapiga kura katika orodha ya wapiga kura lilianza tarehe 11
Oktoba, 2024 na litaendelea hadi tarehe 20 Oktoba, 2024 na tarehe ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa ni 27 Novemba, 2024.
MWISHO
Comments
Post a Comment