Sekunde chache kujiandikisha orodha ya wapiga kura
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Urahisi wa zoezi la kujiandikisha katika
orodha ya wapiga kura umekuwa kivutio kikubwa sana kwa wananchi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, kujitokeza na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024.
Wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma waliojitokeza kushiriki zoezi hilo la uandikishaji wameeleza urahisi wake kuwa halichukui muda mrefu.
Kwa upande wake Mariamu Paul, mkazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Mpunguzi aliwashauri wananchi kujitokeza na kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwasababu zoezi halichukui muda mrefu. Aliongeza kuwa ni haki yao ya msingi na inawapa fursa kubwa ya kuchagua viongozi wa serikali ya mtaa wanaowataka na kuwaasa wasisubiri kuchaguliwa na watu wengine. “Nimekuja kujiandikisha na nawashauri wananchi wengine waje. Nimetumia kama sekunde kadaa tu kwa sababu hata haizidi dakika moja kuandikishwa na haichukui hata muda wako” alisisitiza Paul.
Peter Agustino, mkazi wa Mtaa wa Kigamboni
Nae, Peter Agustino, mkazi wa Mtaa wa
Kigamboni, Kata ya Kikuyu Kaskazini alimpongeza afisa muandikishaji katika Kituo
cha Ofisi yaAfisa Mtendaji Kata ya Kikuyu Kaskazini kwa mapokezi mazuri, huduma
nzuri wanayoitoa na lugha nzuri wanayotumia kupokea wananchi wanaoenda
kuandikishwa. “Mapokezi ni mazuri, wanawakaribisha watu kwa lugha nzuri. Kiukweli
nimefurahia kuhudumiwa hapa, mwandikishaji ni mkarimu mno” alisema Agustino.
Katika hatua nyingine Sylivester Bilingi, mkazi
wa Mtaa wa Muungano, Kata ya Mkonze aliunga mkono juhudi za serikali katika
kuhakikisha kuwa kila mwananchi
aliyekidhi vigezo vya kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa anapata
haki yake ya kuchagua au kuchaguliwa. Alisema, yeye kama mwananchi ataunga
jitihada hizo kwa kutoa muda wake na kwenda kuwahamasisha wananchi kujitokeza
kwa wingi kushiriki zoezi za kujindikisha katika orodha ya mpiga kura. “Nitaongea
na mwananchi mmoja mmoja kumpatia elimu hii niliyoipata ya kujiandikisha katika
orodha ya mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ili na wenyewe
wapate kuelewa umuhimu wa zoezi hili kabla muda wa kujiandikisha haujafika
ukomo” alisema Bilingi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa
kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024 utakaotoa fursa kwa mwananchi kuchagua
mwenyekiti wake wa kijiji, mwenyekiti wa vitongoji vilivyomo katika eneo la
kijiji, wajumbe mchanganyiko wanawake na wanaume pamoja na wajumbe wa kundi la
wanawake ambao idadi yao haitakuwa chini ya theluthi moja ya wajumbe wote wa
halmashauri ya kijiji.
MWISHO
Comments
Post a Comment