Mtoto wa kike apewe fursa ya kuongoza

Na. Faraja Mbise, DODOMA

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Duniani, ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 11, jamii imeaswa kumshirikisha mtoto wa kike katika ngazi ya uongozi tangu anapoanza kukua mpaka anapokuwa mtu mzima.




Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa taasisi ya Msichana Initiatives, Rebecca Gyumi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Lamaiti, Tarafa ya Mndemu, Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma katika Tamasha la Msichana Amani Music Festival.

“Siku hii katika nchi yetu, tunaongozwa na kaulimbiu ya Msichana na Uongozi, Mshirikishe Wakati ni Sasa. Kupitia jukwaa letu la Agenda ya Msichana, tumeitohoa zaidi kaulimbiu yetu ya kitaifa ambapo tunasema Msichana na uongozi, kwakutumia Fursa za Kidijitali au teknolojia ya kidijitali, kwa maana ya kuangalia namna wasichana wanavyoweza kuonesha uongozi kupitia fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye teknolojia ya kidigitali” alisema Gyumi.

Wakati akizungumza na kundi la wananchi na watoto wa kike alisema kuwa, katika kipindi hicho ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ni vizuri kumshirikisha mtoto wa kike katika masuala ya uongozi kwa kuanza pindi tu wawapo shuleni na kwenye klabu zinazohusu masuala ya kijamii.

Kutokana na ripoti ya Jeshi la Polisi nchini Tanzania, inaonesha mwaka 2023 kulikuwa na matukio ya ukatili kwa watoto takribani 15,000 ambayo ukilinganisha na mwaka 2022 matukio yalikuwa 12,000. Kwahiyo, ni sawa na ongezeko la asilimia 25, na makosa hayo unapoyachambua ni makosa ya ubakaji 8,000, ulawiti 2,300 na mimba 1,400.

Gyumi alibainisha changamoto hizo ambazo wanakumbana nazo katika harakati za kumkomboa mtoto wa kike katika wimbi la ukatili wa kijinsia, ambalo ndio changamoto kubwa inayompelekea mtoto wa kike kushindwa kutimiza ndoto zake na kutoa rai kwa jamii kuwalinda watoto wa kike na ukatili wa kijinsia.

“Tukizungumza kuhusiana na masuala ambayo yanamfanya mtoto wa kike ashindwe kuwa kiongozi, hatuwezi kuacha kuzungumzia tamaduni, mila na desturi kandamizi. Kwasababu hatuwezi kuzungumza mtoto wa kike kuwa kiongozi wakati anaozeshwa akiwa na umri wa miaka 12” alisisitiza Gyumi kwa uchungu.

Aidha, alitoa takwimu ya Sensa ya Wat una Makazi ya mwaka 2022 inayoonesha kuwa watoto wa Tanzania ni nusu ya wananchi wote takribani Milioni 29 na kati yao milioni 14 ni watoto wa kike.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Afisa Tarafa ya Mndemu, Isaya Matata, aliishauri jamii kumshirikisha mtoto wa kike katika kumuelimisha stadi za uongozi kwa lengo la kumuandaa kuwa kiongozi bora wa sasa na hapo baadae.

“Lengo mahususi ni kumuandaa mtoto wa kike kuwa kiongozi, tunaposema mabinti zetu wagombee nafasi za uongozi haimaanishi wagombee Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sababu umri wao ni mdogo, hawajafikia hapo bali wanachotakiwa kufanya ni kugombea uongozi katika maeneo yao walipo. Mfano shuleni, makanisani na hata misikitini. Sasa inahimizwa sana kwa watoto wa kike kujitokeza na kushiriki nafasi hiyo, kwa maana hiyo tunamuandaa mtoto wa kike kuwa kiongozi bora wa baadae mwenye kujiamini, kusimama mbele za watu, kuzungumza na kujenga hoja” alisisitiza Matata.

Kwa upande wake Mwalimu wa Shule ya Msingi Lukali, Mwl. Venance Kikoti, alitoa maoni yake katika kuelekea maadhimisho wa siku ya mtoto wa kike duniani kuhusu swala zima la uongozi “wanawake wana haki kama wanaume. Hivyo, washiriki katika mgawanyo wa madaraka katika kugombea” alisema Mwl. Kikoti.

Nae mwanafunzi wa Shule ya Msingi Lamaiti, Sifa Jobumuzenga, alielezea changamoto ambazo zinawafanya washindwe kujitokeza katika kugombea nafasi za uongozi “kuna changamoto nyingi za ukatili wa kijinsia kama ubakaji ni kikwazo kwahiyo tunaomba serikali ikomeshe ukatili wa kijinsia kwa watoto”.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Msichana Initiatives lilidhaminiwa na wadau kutoka kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya jukwaa la msichana wakiongozwa na Flaviana Matata Foundation, M Sema, Tae, Wote sawa, Young strong mothers’ foundation, na grammy. Tamasha lilipambwa na burudani mbalimbali kama nyimbo, mashairi, ngonjera na ngoma kutoka takribani shule za msingi 16 zilizopo katika tarafa ya Mndemu na vikundi vya ngoma kutoka kwa wananchi wa tarafa hiyo.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma