Maafisa Waandikishaji Jiji la Dodoma watakiwa kufungua vituo kwa wakati
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Maafisa
waandikishaji Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuzingatia muda wa
kufungua na kufunga vituo vya uandikishaji orodha ya wapiga kura unaotarajiwa
kufanyika tarehe 11-20 Oktoba, 2024.
Wito
huo ulitolewa katika mafunzo kwa maafisa waandikishaji wa Jiji la Dodoma yaliyofanyika
katika ukumbi wa Mtumba Complex tarehe 08 Oktoba, 2024 na Afisa Uchaguzi
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga.
Akizungumza
na maafisa waandikishaji orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa kuzingatia muda wa kufungua na
kufunga vituo vya kujiandikisha wapiga kura ili kuongeza ufanisi katika
utendaji kazi pindi wawapo katika maeneo yao ya kazi.
“Vituo
vyetu kama mlivyotangaziwa vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa
saa kumi na mbili jioni. Sasa isije ikatokea ukaona hakuna watu ukaweka vitabu
kwenye begi ukaondoka. Sisi tunapita kukagua kila kituo na bahati nzuri kila
kata, kila mtaa kuna mtu anayesimamia huo mtaa. Kwahiyo, kuna mtu atakuwa
anatembea na bodaboda kukagua wewe utamuona kama muandikishwaji ila yupo” alisema
Kasoga.
Aidha,
aliwataka maafisa waandikishaji kutambua sifa za mtu anayepaswa kuandikishwa
kwenye orodha ya daftari la mpiga kura na sifa za mpiga kura baada ya kuandikishwa.
“Kuna
mambo yafuatayo lazima tuyazingatie sana, jambo la kwanza, mtu huyu ni lazima
awe raia wa Tanzania, tunapoenda kufanya kazi zetu lazima tuhakikishe kwamba
kuwa ni raia wa Tanzania, endapo itatokea utamuandikisha mtu ambae siyo raia wa
Tanzania changamoto yake tutakwenda kwenye pingamizi na itakwenda kufanya
marekebisho ya orodha ya wapiga kura. Jambo la pili, awe na miaka 18 na zaidi.
Jambo la tatu ni lazima awe mkazi wa mtaa husika na lazima awe mtu mwenye akili
timamu” alisisitiza Kasoga.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Wakili Cosmas Nsemwa aliwaasa maafisa waandikishaji kutumia lugha
nzuri yenye ukarimu pindi watoapo huduma kwa waandikishwaji katika vituo vyao
vya kazi. Aliongeza kuwa wasitumie lugha ya matusi ambayo itaweza kupelekea
zoezi kuharibika.
“Tuwe
na lugha nzuri kwa wananchi wetu wanaokuja kujiandikisha. Kwahiyo, kutumia hizo lugha zenye matusi na
maudhi ukibainika utakuwa umefanya kosa” alisema Wakili Nsemwa.
Aidha,
kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero, alitoa maelekezo kuhusu vifaa ambavyo
vitatumika wakati wa zoezi la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura na kuwataka
maafisa waandikishaji kutunza vifaa hivyo kwasababu baada ya zoezi vitahakikiwa
baada ya zoezi.
“Unapokabidhiwa
vifaa vya umma na mwisho unayomaliza kuvitumia utahakikiwa. Kwahiyo, tutakapowakabidhi
vifaa, tutakabidhi kwa nyaraka. Kwahiyo, tunategemea kwamba siku ambayo unakuja
kuchukua vifaa, Afisa Mtendaji wa Kata husika na watu wake tutakuwa tunagawa
kata kwa kata ambapo tutakuwa tunauwisha nyaraka hizo kwa kumbukumbu ya
serikali na mkirejesha tutavihakiki kama vifaa vyote vipo ambavyo mmepewa na
vilivyotumika. Kwahiyo, tuhakikishe vifaa vyote vinatunzwa” alisema Odero.
Zoezi
la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura litahusisha vifaa vifuatavyo, daftari
la kuandikia wapiga kura, kalamu, penseli, kifutio, kibao cha wino, tisheti na
kofia, mihuri na mabango ambavyo vinatarajiwa kutolewa tarehe 10 Novemba, 2024
katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Comments
Post a Comment