Jiji la Dodoma wahamasishwa kujiandikisha orodha ya wapiga kura
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Wananchi wamehamasishwa kujitokeza
kwenda kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ifikapo Oktoba 11 hadi 20,
2024 kwa lengo la kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Ushauri huo ulitolewa na Diwani wa Viti
Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asma Karama muda mfupi kabla ya kuanza
kikao cha Kamati ya Mipango miji na Mazingira katika Shule ya Sekondari Umonja
iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Karama ambae ni Naibu Meya Mstaafu wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma alitoa rai kwa wana Dodoma na wananchi wote kwa
ujumla kujitokeza kushiriki katika kujiorodhesha kwenye daftari la wapiga kura kwa
sababu ni muhimu kwa wananchi kutumia haki yao. Alisema kuwa kuwa uchaguzi
utawasaidia kupata viongozi bora.
“Uchaguzi ni gharama, hivyo serikali hugharamia
chaguzi kwa ajili ya kukupa haki wewe mtanzania, ikiwa na maana wanataka
uchague kiongozi unayemtaka sio uchaguliwe kiongozi” alisema Karama.
Pia aliongeza kuwa mwananchi mwenye
sifa za kujiandikisha aende akajiandikishe ili aweze kumchagua kiongozi anayemtaka
na asisubiri kuchaguliwa.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Rosemary Nitwa aliwaomba wananchi wasilalamike uchaguzi
ukiisha bali wajitokeze mapema katika kujiandikisha ili kuchagua viongozi
wanaowataka. Aidha, aliwahamasisha wananchi wenye sifa kwenda kujiandikisha kwenye
orodha ya daftari la wapiga kura.
“Sasa wananchi, nipo hapa nakuomba
uende ukajiandikishe kwenye daftari kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 20, Oktoba,
2024 kwa ajili ya kwenda kupiga kura ya kumchagua mwenyekiti wa serikali ya
mtaa unayempenda na wajumbe wake watano. Ninawaomba sana sana usikae kwa
kulalamika nyumbani kwamba siendi alafu baadae unalalamika kwamba hujapiga kura”
alisema Nitwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment