KADI YA MPIGA KURA SIO LAZIMA KWENYE UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir
Shekimweri, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la
kujiandikisha kwenye orodha ya mpiga kura zoezi litakalofanyika kwa muda wa
siku kumi kuanzia tarehe 11- 20 Oktoba, 2024 na kusema kuwa kadi ya mpiga kura
siyo kigezo cha kupigia kura.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema hayo
alipokuwa akizungumza na mamia ya watumishi wa umma na wananchi waliojitokeza
katika Bonanza la kuhamasisha umma kujitokeza katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa katika Shule ya Sekondari Dodoma iliyopo Mtaa wa National Housing, Kata
ya Makole jijini Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema “hakuna kadi
ya mpiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, siku ya kupiga kura unaweza
kwenda na kitambulisho chochote kile kama leseni ya udereva, kadi ya mpiga kura
ya uchaguzi mkuu, kadi ya bima ilimradi utambulishwe na kadi yoyote. Na kama
hauna kabisa basi hata jirani yako anaeaminika kuwa ni mkazi na ana kadi husika
anaweza kukutambulisha”.
Aidha, aliwataka wananchi wazingatie
muda wa kujiandikisha uliowekwa ili kusiwepo na malalamiko yoyote kwasababu muda
wa kuorodhesha majina katika orodha ya mpiga kura hautaongezwa. pia alisisitiza
Uchaguzi wa serikali ngazi ya mitaa ni mchakato wa kidemokrasia.
“Tunategemea uandikishwaji utafanyika
kwa haraka na kwa kasi. Kwahiyo, muda uliowekwa wa uandikishaji unaonekana ni
mrefu tukijipanga vizuri. Ndio tukaanza na bonanza hili ili tupeane elimu tukianza
na watendaji pamoja na wenyeviti wa mitaa, tunataka mtumie nguvu nyingi kadri
inavyowezekana mwanzoni ili mwishoni iwe ni kumalizia” alisema Alhaj Shekimweri.
Akiongelea tofauti kati ya zoezi
uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura na uchaguzi wa serikali za mitaa
alifafanua utofauti wake. “Uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura
ulihitaji mtu ambae alishashiriki uchaguzi uliopita au mpiga kura ambae hakuwampiga
kura. Kwahiyo, kama ni wazamani ana kadi yake labda iliharibika au kupotea
alikuwa anakwenda kuboresha taarifa zake tofauti na Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa maafisa watakaokuwa wanaandikisha hawatatumia mashine za BVR (Biometric
Voters Registration) watakuwa na madaftari ya kusajili wapiga kura” aliongeza Alhaj
Shekimweri.
Aidha, alipongeza timu ya Uchaguzi
ikiongozwa na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick
Sagamiko, kwa kazi nzuri ya uhamasishaji wanayoendelea kuifanya tangu zoezi la
kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura mpaka sasa kuelekea
katika zoezi la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwa ajili ya
uchaguzi utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Bonanza la kuhamasisha umma kushiriki
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa liliongozwa na kaulimbiu ‘Serikali za
Mitaa, Sauti ya Wananchi, Tujitokeze Kushiriki Uchaguzi’ lilihudhuriwa na watumishi mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, taasisi mbalimbali na mamia ya wananchi
likipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari
Dodoma na Chinangali, walimu wa shule za msingi na sekondari, wanamuziki kutoka
Dodoma Extra Sound na Dodoma One Theatre. Michezo iliyochezwa ni mpira wa
miguu, bao, drafti, kukumbiza kuku, kuvuta kamba, kukimbia na yai pamoja na
kukuna nazi.
MWISHO
Comments
Post a Comment