Uzinduzi ujenzi jengo la mapumziko Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
Na. Asteria Boniface, DODOMA
MBUNGE wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony
Mavunde amezindua ujenzi wa jengo la mapumziko la wananchi Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Dodoma na kusema kuwa ujenzi huo ni sadaka yake kwa wananchi.
Alisema kuwa nje ya jengo hilo kuna eneo
ambalo wanakaa wananchi ambao asilimia kubwa hawaishi katika Jiji la Dodoma na
wanatumia sehemu ile kama sehemu ya kupumzikia kwaajili ya kusubiri muda wa
kuwaona wagonjwa wao. Aliongeza kuwa wapo baadhi ambao hawana sehemu ya kulala
na hawana makazi Dodoma na hawawezi kurudi walipitoka kwasababu ni mbali.
Mbunge huyo alisema kuwa wakati mwingine wakina
mama, baba na watoto wanachanganyikana na kulala sehemu moja. Alisema kuwa
kulingana na maadili ya kitanzania sio vema sana kuchanganyika watu wa jinsi
tofauti sehemu moja na hasa ambao kwa namna moja au nyingine hawana uhusiano
wowote. “Mimi kama Mbunge, jambo hili lilinigusa sana nikasema moja ya sadaka,
Mungu akinijalia na nitapenda niiache kama alama ni kiwahifadhi na kiwastiri wananchi
wangu ambao wanakaa katika eneo lile ambalo lipo wazi. Nikasema nitalifanyia
kazi na leo ndugu zangu nimezindua rasmi ujenzi wa jengo la kisasa kabisa na
wananchi wa ndani na nje ya Dodoma watapata sehemu nzuri ya kupumzika” alisema
Mavunde.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Dodoma, Dkt. Sara Ludoviki alitoa taarifa fupi kuhusu hospitali hiyo na
kueleza changamoto wanazopitia katika baadhi ya majengo yanayotoa huduma
hospitalini hapo.
Alisema kuwa hospitali hiyo ina miaka 104 na
ilianza kama kituo cha afya na imekua na kufikia hadhi ya kuwa hospitali ya
Mkoa kwa tangazo la serikali toleo namba 46 la tarehe 12 Novemba, 2010. Aliongeza
kuwa hospitali inatoa huduma kwakupitia sera, miongozo na taratibu zilizowekwa
na Wizara ya Afya.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea madaktari bingwa 31. Nusu ya madaktari
hao, wamepatikana katika awamu hii ya sita. Mafanikio tuliofikia ni kwa upande
jengo la uzazi kwa kupunguza vifo vya wamama wajawazito na watoto kwa kuwekwa
kwa huduma mbalimbali kama sehemu ya uangalizi wa wagonjwa mahututi ya watoto
na pia katika idara ya mionzi tumewekewa ‘CT scan’" alisema Dkt. Ludoviki.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma inauwezo
wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 1,500 kwa siku moja ambao ni mchanganyiko wa
wagonjwa wa nje na walio lazwa na wengine wanaotoka katika mikoa jirani.
MWISHO
Comments
Post a Comment