Elimu Sekondari yafanya usafi Kituo cha Afya Makole

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

DIVISHENI ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeadhimisha maadhimisho ya kuelekea kilele cha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya usafi katika Kituo cha Afya Makole kwa lengo la kuwawekea mazingira safi na salama wagonjwa wanaopata huduma kituoni hapo.

Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Zainabu Abdallah akiongea na mamia ya walimu, wanafunzi na Jumuiya ya Kituo cha Afya Makole


Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Zainabu Abdallah alipokuwa akiongea na mamia ya walimu, wanafunzi na jumuiya ya wafanyakazi wa Kituo cha Afya Makole kufanya usafi katika kituo hicho.

Mwl. Abdallah alisema “sisi Divisheni ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumeamua kuadhimisha maadhimisho ya kuelekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya usafi katika Kituo cha Afya Makole. Kama mnavyofahamu Makole ni kituo cha afya cha kimkakati kinachohudumia watu wengi, tumeona ni busara kushiriki zoezi la usafi wa mazingira. Hapa tumekuja walimu na wanafunzi wa shule za sekondari zilizo karibu na kituo hiki kufanya usafi. Tunafanya usafi kwa sababu ni muhimu katika maisha yetu na tunawafundisha watoto wetu tabia ya kupenda usafi. Hospitali ni moja ya sehemu muhimu inayotakiwa kuwa safi na mazingira yakuvutia kwa wanaopata na kutoa huduma”.

Alisema kuwa zaidi ya zoezi la usafi, maadhimisho hayo yamewakutanisha walimu kwa walimu na wanafunzi kwa wanafunzi kuungana na kuwa wamoja kwa kufanya usafi wa pamoja.

Akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Afisa Tarafa ya Dodoma mjini, Zainabu Mabuye alisema kuwa siku hiyo imekuwa na shughuli nyingi za kijamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanzania. “Mfano hapa Makole tunafanya usafi kwa kushirikiana na Divisheni ya Elimu Sekondari Jiji la Dodoma na walimu na wanafunzi wa sekondari. Zoezi hili pia linafanywa na Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma kule Shule ya Msingi Dodoma Mlimani na Amani kwa kupanda miti ya aina mbalimbali na baadae kufuatiwa na bonanza la michezo katika uwanja wa Shule ya Sekondari Dodoma. Pia kutakuwa na zoezi la uchangiaji damu litakaloanza muda mfupi ujao ni zoezi muhimu kwa kila mmoja wetu kushiriki” alisema Mabuye.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ambae ni Afisa Tarafa ya Dodoma mjini, Zainabu Mabuye akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya


Alisema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeandaa mkesha mkubwa katika Shule ya Msingi Makole tarehe 25 Aprili, 2024. “Nichukue nafasi hii kuwaalika wananchi wate kwenye mkesha mkubwa kesho kuanzia saa 11 jioni mpaka saa 6 usiku. Burudani mbalimbali zitakuwepo, wajasiriamali watakuwa wakionesha bidhaa zao nyama choma za kutosha, usijaribu kukosa” alisema Mabuye.

Kwa upande wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma, Husna Juma alisema “Tupo hapa Kituo cha Afya Makole tunaadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na tumekuja kusaidia usafi ili kuboresha afya zetu, kuboresha mazingira na kupunguza hewa chafu katika anga”.



Ikumbukwe kuwa zoezi la usafi zimeratibiwa na divisheni ya elimu sekondari likijumuisha kufanya usafi katika vituo vingine vya afya vilivyopo nje kidogo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma