Ujenzi wa Shule ya Sekondari Miyuji B waweka historia
Na. Mwandishi Wetu,
SERIKALI
ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka
historia kwa kujenga Shule ya Sekondari Miyuji B na kuwasaidia wanafunzi
waliokuwa wakitembelea umbali mrefu kufuata elimu katika Kata ya Mnadani.
Mwl. Fredrick Mwakisambwe akielezea shule ya Sekondari Miyuji B
Kauli
hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Mwl.
Fredrick Mwakisambwe alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea
shule hiyo kujionea mafanikio ya miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita
katika Shule mpya ya Sekondari Miyuji B iliyopo Kata ya Miyuji jijini Dodoma.
Mwl.
Mwakisambwe ambae pia Afisa Elimu Vifaa na Takwimu katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma alisema kuwa shule hiyo imekamilika ikianza na wanafunzi wa kidato
cha kwanza. “Ni mara ya kwanza katika hitoria ya Kata ya Miyuji kuwa na shule
ya sekondari. Watoto wameteseka kwa muda mrefu kutembea umbali mrefu kufuata
huduma ya elimu. Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
mwaka jana 2023 alitupatia shilingi 544,000,000 kujenga shule hii ya kisassa
kabisa yenye madarasa nane, maabara tatu, jengo la utawala, jengo la TEHAMA na
matundu ya vyoo” alisema Mwl. Mwakisambwe.
Akiongelea
mchango wa shule hiyo katika kukuza taaluma, alisema kuwa itasaidia kuongeza
kiwango cha ufaulu. “Ni jambo la kipekee kwetu sisi wasimamizi wa elimu katika Jiji
la Dodoma kwasababu tulikuwa tukipata shida sana katika usimamizi wa taaluma. Lakini
uwepo wa shule hii unaongeza chachu kwa watoto kuweza kusoma vizuri, utoro
utapungua na utulivu kwa watoto wetu utakuwepo. Tunamshukuru sana mheshimiwa
Rais kwa kipindi hiki cha miaka mitatu katujengea shule nyingi na hii ni moja
wapo” alisema Mwl. Mwakisambwe kwa sauti ya shukrani.
Muonekano wa Shule ya Sekondari Miyuji B
Akiongelea
faida ya kujengwa Shule mpya ya Sekondari Miyuji B, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl.
Clara Mwinshehe alisema kuwa ni ukombozi kwa wanafunzi. “Faida ya kujengwa kwa
shule hii ni wanafunzi wengi walikuwa wakipata changamoto kutoka eneo hili
kwenda Kata ya Mnadani umbali wa kama kilometa saba kutoka hapa. Jambo ambalo
lilikuwa linasababisha watoto wakike kushindwa kumaliza masomo kwa changamoto
za mimba kutokana na kutembea umbali mrefu. Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais
kwa kuleta hii shule Mtaa wa Mpamaa, Kata ya Miyuji inawanufaisha wanafunzi na
watafanya vizuri zaidi kwenye masomo yao kwasababu imewapunguzia kutembelea
umbali mrefu kufuata elimu. Mungu akubariki sana mama, tunakushukuru kwa miaka mitatu,
tunakupongeza” alisema Mwl. Mwinshehe kwa furaha.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpamaa, Happy Joshua alisema kuwa shule hiyo
ni muhimu kwa wananchi wake. “Napenda kumshukuru mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa
mradi huu mkubwa wa shule ya sekondari maana katika Kata ya Miyuji hatukuwa na
shule ya sekondari. Pia niwashukuru wananchi wa Mpamaa kwa kujitoa kwao katika
mradi huu. Manufaa ya mradi huu ni watoto wetu hawatatembea tena umbali mrefu
kufuata elimu” alisema Joshua.
MWISHO
Comments
Post a Comment