Rais Dkt. Samia atoa shilingi 544,225,626 ujenzi shule ya Sekondari Michese
Na. Dennis Gondwe, MKONZE
RAIS,
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha shilingi 544,225,626 kujenga Shule mpya
ya Sekondari Michese ili kupunguza msongamano katika Shule ya Sekondari Mkonze
na kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu.
Muonekano wa Shule ya Sekondari Michese
Kauli
hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Fredrick Mwakisambwe alipoongoza waandishi
wa habari kutembelea Shule mpya ya Sekondari Michese iliyojengwa katika Kata ya
Mkonze jijini Dodoma.
Mwl.
Mwakisambwe ambae ni Afisa Elimu Vifaa na Takwimu katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma alisema “ndugu waandishi wa habari, tupo Kata ya Mkonze eneo la Michese.
Eneo hili ni moja ya maeneo yaliyonufaika na kujengwa shule mpya ya sekondari. Kata
ya Mkonze ina idadi kubwa ya wananchi na kwa muda mrefu ilikuwa na shule moja
ya sekondari ya kata. Mwaka huu 2024 idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga
kidato cha kwanza katika kata ilikua ni wanafunzi 700. Idadi hiyo ni kubwa kuhudumiwa
kwenye shule moja ya Sekondari Mkonze. Hivyo, serikali ya Dkt. Samia Suluhu
Hassan imeweza kutuletea fedha shilingi 544,225,626 kujenga majengo haya
yanayoonekana mazuri na ya kisasa. Madarasa nane, Maabara tatu, jengo la Maktaba,
jengo la TEHAMA, jengo la Utawala na matundu ya vyoo”.
Mwl. Fredrick Mwakisambwe akielezea umuhimu wa Shule ya Sekondari Michese
Alisema
kuwa shule hiyo itasaidia mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi na
kufundishia kwa walimu. “Kwa kipekee kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma
na halmashauri tunashukuru sana juhudi hizi na watoto watasoma katika shule hii
kwa umbali usio mrefu sana. Tunaipongeza sana serikali kwa uwekezaji huu
mkubwa. Na sisi tunaahidi kusimamia taaluma katika Jiji la Dodoma ili juhudi
hizi tusimuangushe mheshimiwa Rais” alisema Mwl. Mwakisambwe kwa kujiamini.
Msimamizi
wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Michese, ambae ni Mkuu wa Shule ya
Sekondari Mkonze, Mwl. Andrew Rumishael alisema kuwa Kata ya Mkonze ni kubwa
ilihitaji shule mpya muda mrefu kwa sababu iliyopo ilizidiwa wingi wa
wanafunzi. “Kulikuwa na idadi kubwa sana ya wanafunzi wanaoishi Michese
waliokuwa wakitembelea kuifuata Shule ya Sekondari Mkonze. Shule hii itapunguza
umbali wa karibu kilomita nane walizokuwa wakitembea wanafunzi kwenda na kurudi
na kufanya wawe na nguvu ya kutulia na kusoma vizuri na hata ufaulu wao utaongezeka
kwa sababu ya kupunguza umbali huo wa kutembea” alisema Mwl. Rumishael.
Aliongeza
kuwa shule hiyo itasaidia kumlinda mtoto wa kike kumaliza masomo yake dhidi ya
changamoto za mimba. “Shule hii itamsaidia mtoto wa kike kuzingatia masomo yake
na kufikia malengo yake. Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kujali
elimu na kumlinda mtoto wa kike na kuhakikisha anatimiza malengo yake” alisema
Mwl. Rumishael.
Kwa
upande wa mkazi wa Michese Isaya Halwa alipongeza maono ya Rais ya kuboresha
mazingira ya elimu kwa watoto katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Hapo awali
watoto wetu walikuwa wanasoma mbali na na elimu ilikuwa shida sana. Tunamshukuru
Mungu sababu ya maono na kujituma kwake kuanngalia mazingira ya wananchi wanachohitaji.
Mheshimiwa Rais ameona aanze kuandaa kizazi bora cha kesho, sasa tunaona mwanga
ambao hatukuwa tukiuona hapo awali” alimalizia Halwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment