LTIP Yatambua Vipande vya Ardhi 11,000 Nzega
Na Magreth Lyimo, WANMM
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa
Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi umetambua vipande vya ardhi takribani 11,000 katika
Halmashauri ya Mji wa Nzega ikiwa lengo ni kutambua takribani vipande 20,000.
![]() |
Kiongozi wa Timu inayotekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Bw. Nolasko Matsuva akielezea namna mradi huo unavyotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora |
Hayo yalisemwa Nolasko Matsuva,
Kiongozi wa Timu inayotekeleza mradi huo katika halmashauri ya mji wa Nzega
Mkoani Tabora wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji
wa Mradi huo.
‘‘Katika Halmashauri ya Mji wa
Nzega utekelezaji wa Mradi ulianza na shughuli za uwandani Desemba 5,
2023 katika Mtaa wa Maporomoko, Uwanja wa ndege, Upiriri, Ushirika, mpaka sasa
tuko mtaa wa Nyasa ambapo tumetambua vipande vya ardhi takribani 11,000’’
alisema Matsuva.
Katika mwitikio wa wananchi
kushiriki zoezi hilo, Matsuva amesema wamefanikiwa kutambua vipande 11,000 kwa
muda mfupi kwa kuwa walipata ushirikiano mkubwa wa wananchi wa Nzega pamoja na
Viongozi wao hatua ambayo imerahisisha zoezi hilo kwenda kwa kasi na ufanisi
mkubwa.
Matsuva alisema wananchi wametambua
umuhimu wa kupimiwa maeneo na kutoa wito kwa wakazi wa Nzega kuendelea
kujitokeza kwa wingi ili kukamilisha zoezi hilo na kuhimiza kila mmiliki
awepo katika eneo lake wakati wa zoezi la utambuzi ili kutoa taarifa sahihi.
‘‘Naishukuru Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuuleta mradi huu hapa Nzega, utasaidia sana
kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuwa takribani asilimia 99 ya Nzega magharibi
na Nzega mashariki itakuwa imepimwa’’ alisema Matsuva.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo
katika Halmashauri ya Mji wa Nzega amekiri kuwa mradi huo umewafikia kwa wakati
muafaka na utasaidia kuongeza thamani ya maeneo yao pindi watakapomilikishwa
Kisheria.
Nae Meneja wa Urasimishaji Mjini, Leons
Mwenda alisema mradi huo umedhamiria kutoa takribani hati miliki 1,500,000
katika maeneo ya mjini ambapo mpaka sasa zoezi la upangaji, upimaji na
umilikishaji linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini kama Halmashauri
ya Wilaya ya Chalinze, Halmashauri ya Mji wa Nzega, Halmashauri ya Manispaa ya
Kahama, Shinyanga, Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambapo jumla
ya vipande 50,000 vimetambuliwa katika maeneo hayo kuanzia mwezi Julai 2023
hadi Januari 2024.
Aliongeza kuwa zoezi hilo
linatarajiwa kuendelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na
Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Peramiho.
Aidha, jumla ya Halmashauri 22
zinatarajiwa kuongezwa katika utekelezaji wa mradi huo ifikapo mwezi Aprili
mwaka huu ambapo kazi ya upangaji, upimaji na umilikishaji zitafanywa na
makampuni binafsi ili kuongeza kasi ya kumfikia kila mlengwa kwa wakati.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa
Milki za Ardhi unatekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kwa muda wa miaka mitano (2022 – 2027) ambapo lengo lake kuu ni kuongeza
usalama wa milki za ardhi nchini.
![]() |
Meneja Msaidizi wa Urasimishaji Mijini, Martin Orden akitoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Utemini katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora |
![]() |
Afisa Mradi akichukua taarifa muhimu za umiliki kwa mkazi wa Mtaa wa Utemini katika Halmashauri ya Mji wa Nzega Mkoani Tabora wakati wa zoezi la kutambua vipande vya ardhi katika mtaa huo |
Comments
Post a Comment