Bazara la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha rasimu ya Mpango na Bajeti shilingi 146,287,642,299 kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
BARAZA
la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limepitisha rasimu ya mapendekezo
ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya shilingi
146,287,642,299.70 ikitajwa kuwa ni bajeti ya wananchi.
![]() |
Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, Francis Kaunda akiwasilisha rasimu ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 |
Akiwasilisha
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma mapendekezo ya rasimu ya Mpango na
Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Jiji la Dodoma Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, Francis
Kaunda alisema kuwa bajeti hiyo imelenga kutatua changamoto za wananchi.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmasahuri ya Jiji la
Dodoma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni jumla ya shilingi 146,287,642,299.70.
Kati ya fedha hizo, shilingi 58,521,926,299.70 ni mapato ya ndani, shilingi
73,852,812,000 ni ruzuku ya mishahara, shilingi 1,168,778,000 ruzuku ya
matumizi mengineyo na shilingi 12,744,126,000 ni ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Hivyo, bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 imeongezeka kwa 14.4% ukilinganisha
na bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024” alisema Kaunda.
Mwenyekiti
wa mkutano huo ambae ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof.
Davis Mwamfupe alisema kuwa bajeti hiyo imemlenga mwananchi wa kawaida moja kwa
moja. “Ndiyo maana tukaweka mkazo mkubwa katika sekta ya elimu na sekta ya
afya. Mfano katika elimu ya msingi tumeweza kuongeza vyumba vya madarasa 76, katika
sekondari maabara 15 zimekamilika mpaka sasa. Katika miradi tumejikita zaidi
kuhakikisha miradi viporo ndiyo inakuwa ya kipaumbele ili kuunga juhudi za
wananchi katika maeneo ya pembezoni mwa halmashauri yetu” alisema Prof.
Mwamfupe.
Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Maduhu Ilanga alisema kuwa timu
yake ya wataalam imejipanga vizuri kutekeleza bajeti hiyo. “Mheshimiwa
Mwenyekiti nikuhakikishie kwamba tumejipanga, tupo na timu nzuri ya wakuu wa
divisheni na vitengo pamoja na watendaji wengine. Bahati nzuri tumejipangia
malengo na tumepeana mikataba. Kwa hiyo nikuhakikishie kilichopitishwa na
baraza lako na ushauri uliotolewa tutakwenda kuutekeleza kwa weledi mkubwa.
Tutakusanya kila shilingi ambayo tumeipitisha kwa weledi. Tutakusanya kwa
kuwapa elimu wananchi ili walipe kodi wakielewa haya ndiyo maendeleo yao”
alisema Ilanga.
Akichangia
katika rasimu hiyo, Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira aliitaja
bajeti hiyo kuwa inagusa wananchi moja kwa moja. “Mimi niwashukuru wataalam
wetu kutuandalia rasimu ya bajeti hii nzuri, kupitia vikao vyetu mbalimbali
madiwani walishauri maeneo kadhaa na kuelekeza fedha ziende kwenye miradi ya
maendeleo inayogusa wananchi moja kwa moja. Kufanya hivyo, tutahakikisha kero
katika kata zinatatuliwa katika mwaka wa fedha 2024/2025” alisema Fundikira.
Kwa
upande wake, Diwani wa Kata ya Kilimani, Neema Mwaluko alisema bajeti ni nzuri
nakusisitiza ukusanyaji wa mapato ili kuitekeleza bajeti hiyo. “Mheshimiwa
Mwenyekiti kupanga bajeti ni kitu kingine na utekelezaji ni kitu kingine.
Waswahili wanasema kidole kimoja hakivunji chawa, ili tukaitekeleza bajeti hii
vizuri ndugu madiwani na wataalam twende tukaungane ili tuweze kukusanya mapato
yatakayoweza kutekeleza bajeti hii” alisisitiza Mwaluko.
MWISHO
Comments
Post a Comment