Wilaya ya Dodoma yatoa zawaid kwa waliojifungua Kituo cha Afya Makole kuelekea Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara
Na. Dennis Gondwe, MAKOLE
MIAKA
62 ya Uhuru wa Tanzania Bara Wilaya ya Dodoma imewapatia zawadi kina mama
waliojifungua katika Kituo cha Afya Makole na kuwatakia heri na kuwahakikishia
kuwa serikali inataendelea kutoa huduma bora kwao.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabi Shekimweri akimkabidhi zawadi mama aliyejifungua katika Kituo cha Afya Makole jijini Dodoma |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipoongoza
timu ya wataalam wa wilaya na halmashauri kukagua hali ya huduma katika Kituo
cha Afya Makole, kutembelea kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua
na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Alhaj
Shekimweri alisema kuwa Wilaya ya Dodoma katika kuelekea maadhimisho ya miaka
62 ya Uhuru wa Tanzania Bara imetembelea Kituo cha Afya Makole kukagua hali ya
utoaji huduma. “Kwa niaba ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tumekuja kuona
huduma zinatolewaje hapa sehemu ya kujifungulia. Tunafahamu hapa kuna wastani wa kujifungua
kawaida wanawake kati ya 15-25 kwa siku na wale wanaojifungua kwa upasuaji ni
kati ya 4-6 kwa siku. Hii ni idadi kubwa hivyo, tuna hamu ya kupata mrejesho wa
huduma hizo. Lakini pia kuwaletea zawadi ndogo ya kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru
wa Tanzania bara tukiamini kuwa uhuru huu siyo tu wa kujitawala lakini wa
kujiletea maendeleo. Kina mama wajawazito kupata huduma nzuri za kliniki
wakielekea kujifungua, wajifungue katika maeneo salama katika vituo vya kutolea
huduma kama hapa Kituo cha Afya Makole. Na haya ndiyo matunda ya uhuru wetu”
alisema Alhaj Shekimweri.
Alisema
kuwa Rais, amefanya mambo makubwa katika sekta ya Afya. “Mheshimiwa Rais, anatujengea
hospitali ya wilaya, tayari ametuletea shilingi 1,500,000,000 za kujenga
hospitali hiyo na hapa Makole ametuletea shilingi 750 za kuboresha huduma za
Afya. Tumekuja kuwasalimia na tunaendelea kuwaombea heri kwa Mungu na
tunawapenda na tunawathamini na tupo hapa kuonesha upendo huo” alisema Alhaj
Shekimweri.
Akitoa
taarifa fupi ya huduma kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mganga Mkuu wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa watu wengi wanapenda
kujifungua katika Kituo cha Afya Makole kutoka na ubora wa huduma. “Tumekuwa
tukipata kina mama takribani 20 wanaojifungua kila siku katika kituo hiki.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kama ulivyoona kuna kimama takribani 47 waliolazwa na
waliojifungua katika kituo hiki. Tunashukuru tunapopata matokeo kuwa
wanajifungua salama ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kuona kina mama wanajifungua salama lakini na watoto wao wakiwa salama” alisema
Dkt. Method.
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method akikabidhi zawadi kwa mama aliyejifungua katika Kituo cha Afya Makole |
Kwa
upande wa mama aliyejifungua katika kituo hicho, Stella Gilbert alisema huduma
ni nzuri. “Nimejifungua leo saa sita mchana katika Kituo cha Afya Makole tena
nimejifungua salama mtoto wa kiume. Nawashukuru madaktari na wauguzi
wanahudumia vizuri na wanajali sana wagonjwa, Mungu awabariki sana. Hali ya
huduma ni nzuri sana” alisema Gilbert.
Katika
kuelekea miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Dodoma ilitembelea Kituo
cha Afya Makole kukagua hali ya utoaji huduma katika wodi ya kima mama, kuwatia
moyo kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua na kuwapatia zawadi
mbalimbali.
Comments
Post a Comment