Serikali ya Dkt. Samia inawajali wafanyakazi wa Sekta ya Afya
Na. Dennis Gondwe, MAKOLE
SERIKALI
ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali wafanyakazi
wa sekta ya Afya na kuthamini huduma wanazotoa kwa wananchi katika kuelekea
kipindi cha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akiongea na waandishi wa habari |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa
akiongea na wafanyakazi wa Kituo cha Afya Makole katika kuelekea kilele cha
miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Alhaj
Shekimweri alisema “tunaposherehekea Uhuru wa nchi yetu, hawa wanaohudumiwa ni
watanzania wenzetu ambao wapo huru. Hivyo, tunawajibu wa kuwasaidia ili
wajifungue wakiwa salama na wengine wanaopata huduma mbalimbali za Afya.
Serikali ya awamu ya sita inawajali na milango yetu ipo wazi kuwasikiliza pale
mtakapohitaji kusikilizwa. Najua Mganga Mkuu, Dkt. Andrew Method anafanya kazi
vizuri na sisi tunamtegemea sana na anawaunganisha vizuri. Najua mpo salama
kwenye mikono yake na Mganga Mfawidhi, Dkt. Revocatus Baltazar. Nachukua nafasi
hii kutambua, kuthamini na kuwapongeza kwa kazi nzuri, hongereni sana”.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akikabidhi zawadi kwa mama aliyejifungua |
Aidha,
alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye sekta
ya Afya kuanzia mishahara, miradi, vifaa tiba, kinga na vitendanishi. “Ukiwa
taifa huru moja ya mambo yanaoonesha ni uwezo wa kutibu wananchi wako. Nimefika
hapa kuwaona wagonjwa kina mama waliojifungua na tumepata mrejesho wa huduma
nzuri na wanazifurahia. Ukiona wanafurahia hizi huduma hazifanywi na roboti
zinafanywa na wanadamu ambao ndiyo ninyi. Niwaombe muendelee na huduma hizo
mnazotoa kwa weledi na upendo” alisema Alhaj Shekimweri.
Katika
kuelekea miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Dodoma ilitembelea Kituo
cha Afya Makole kukagua hali ya utoaji huduma katika wodi ya kima mama, kuwatia
moyo kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua na kuwapatia zawadi
mbalimbali.
MWISHO
Comments
Post a Comment