KAMATI YA SIASA WILAYA YA DODOMA YAPONGEZA UJENZI KITUO CHA AFYA ILAZO
NA. Dennis Gondwe, ILAZO
KAMATI
ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma imeridhishwa na hatua ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo
unaoendelea na kusema kuwa wilaya inaoga maendeleo.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma wakikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo |
Kauli
hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma,
Charles Mamba alipoongoza Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma kutembelea na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo kinachojengwa jijini
Dodoma.
Mamba
alisema “nianze kwa kumshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuitendea
mema Dodoma hasa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Sisi tunaoga maendeleo. Kata ya
Nzuguni, Ipagala na kata za jirani. Mradi huu ni wenu na ni jukumu lenu
kuutunza ili uwe endelevu”.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya
Dodoma, Shaban Shaban alisema kuwa wasimamiz wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo
wapo makini. “Kwa jinsi tulivyoukagua tu mradi tumeona kuta zimenyooka vizuri
na msingi umejengwa kwa kiwango bora kabisa. Mheshimiwa Rais, anapotoa fedha
anataka kuona zinatumika vizuri. Bila usimamizi mzuri hatuwezi pata
kilichokusudiwa. Pongezi kwa usimamizi wako Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, sisi kama
vijana tutarudi hapa kwa sababu vijana wa CCM hii ndo miradi ya kutembelea
kwenye kata. Umoja wa vijana wa CCM hizi ndizo kazi zetu kusimamia na uadilifu”
alisema Shaban.
Akisoma
taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo, Mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni
ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Goodluck
Magoti alisema kuwa lengo la ujenzi wa kituo hicho ni kuboresha huduma za mama
na mtoto na huduma za upasuaji.
Mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Goodluck Magoti |
Alisema
kuwa jengo la mama na mtoto ujenzi wa lenta umekamilika. “Jengo la wagonjwa wa
nje jamvi limekamilika hatua ya kupandisha kuta inafuata. Jengo la Maabara lipo
kwenye hatua ya kufunga lenta. Jengo la wodi ya wazazi, jamvi limekamilika
hatua inayofuata ni kupandisha kuta. Majengo mengine ni la upasuaji lipo kwenye
hatua ya upangaji mawe. Jengo la kuhifadhia maiti lipo kwenye hatua ya lenta na
jengo la kufulia lipo kwenye hatua ya lenta” alisema Magoti.
Aliongeza kuwa halmashauri imepokea baadhi ya vifaa tiba kwa ajili ya kituo hicho. Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vifaa vya chumba cha upasuaji na majenereta mawili.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri akisisitiza jambo
Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa kituo hicho
kitakuwa kikubwa chenye hadhi ya hospitali ya wilaya. Alisema kuwa ujenzi wa
kituo hicho ni matokeo ya ziara za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan nje ya nchi
na kukuza diplomasia ya kiuchumi.
Ikumbukwe
kuwa Kituo cha Afya Ilazo kinajengwa na Mkandarasi Salem Construction Ltd kwa
gharama ya shilingi 2,800,000,000 chini ya ufadhili wa KOICA kupitia Shirika la
kuhudumia Watoto UNICEF kikitarajia kuhudumia wananchi 99,743 wa Kata ya
Nzuguni na Ipagala.
MWISHO
Comments
Post a Comment