KAMATI YA SIASA KATA YA MSALATO YATAKIWA KUSIMAMIA MIRADI
Na.
Dennis Gondwe, MSALATO
KAMATI
ya Siasa ya Kata ya Msalato imetakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya
maendeleo inayotekelezwa katika kata ili kujiridhisha ya thamani ya fedha.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma, Charles Mamba alipoongoza Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma kutembelea na kukagua ujenzi wa mabweni mawili, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato iliyopo Kata ya Msalato jijini hapa.
Mamba
alisema kuwa Kamati ya Siasa Kata ya Msalato ina wajibu wa kufuatilia na
kusimamia miradi yote ya maendeleo inayotekelzwa katika kata hiyo. “Kamati ya
Siasa Kata ya Msalato mradi huu ni wa kwenu, msisubiri Kamati ya Siasa Wilaya ya
Dodoma kuja kukagua. Lazima muwe mnapanga ratiba zenu kukagua miradi hii.
Serikali ya awamu ya sita inaleta fedha nyingi kwenye kata kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo, jukumu lenu ni kusimamia utekelezaji wake na
thamani ya fedha ionekane katika miradi hiyo” alisema Mamba kwa msisitizo.
Akisoma
taarifa ya ujenzi wa mabweni mawili, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya
vyoo kwa Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma Mkuu wa Shule ya Sekondari ya
Wasichana Msalato, Mwl. Mwasiti Msokola alisema kuwa shule yake ilipokea
shilingi 428,000,000 kutoka serikali kuu. “Fedha hizo zilikuja kwa ajili ya
ujenzi wa mabweni mawili, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo. Lengo
la mradi huu ni maandalizi ya kuwapokea wanafunzi 452 wa kidato cha tano mwaka
2023. Ujenzi huu unatekelezwa kwa kutumia utaratibu wa ‘force account’ ambapo
kamati tatu ziliundwa za ujenzi, manunuzi na mapokezi ili kusimamia utekelezaji
wa mradi huu” alisema Mwl. Msokola.
Mkuu
huyo wa shule alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha
hizo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. “Miundombinu hii itasaidia kupunguza
upungufu wa mabweni, madarasa na matundu ya vyoo shuleni hapa. Kipekee tunatoa
shukrani za dhati kwa ushirikiano wa karibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kamati ya
Usalama Wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji
pamoja na uongozi wa Kata ya Msalato, walimu wote na kamati za utekelezaji
mradi huu” aliongeza.
Awali
akimkaribisha Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj
Jabir Shekimweri alisema kuwa Shule ya Wasichana Msalato ni shule maalum inayochukua
wanafunzi na walimu wenye vipaji toka nchi nzima. “Tunaendelea kuwapa nguvu na
kuwatia moyo Shule ya Sekondari ya Sasichana Msalato kwa sababu wilaya
tunawategemea kwenye ufaulu na kuipaisha Wilaya ya Dodoma” alisema Alhaj
Shekimweri.
MWISHO
Comments
Post a Comment