AWAMU II YA KLINIKI YA ARDHI JIJI LA DODOMA KUTATUA MIGOGORO KATA KWA KATA

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendesha Kliniki ya Ardhi kwa lengo la kutatua migogoro ya Ardhi na kuwaondolea kero wananchi.


Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akitoa taarifa ya katibu katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea taarifa za utendaji kazi kwa kamati za kudumu za halmashauri kwa kipindi ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kayombo alisema “baada ya Kliniki ya Ardhi ya kwanza kufanikiwa vizuri, tumeendelea na kliniki ya pili iliyoanza Jumamosi tarehe 4 Novemba na itaendelea hadi tarehe 20 Novemba, 2023. Tumepanga watu kikata, kwa siku tunasikiliza na kuhudumia kata nne. Baada ya tarehe 20 tutajipima tena kuona tumefanikiwa kiasi gani na kama watu bado wanashida zoezi litakuwa endelevu. Tunaishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakurugenzi wake wote, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi wametoka ofisini tumeungana nao kwenye Kliniki ya Ardhi Dodoma”.

Aidha, aliwaomba madiwani kuwahimiza wananchi wenye changamoto za Ardhi kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo kwa kuzingatia ratiba ya kata husika. “Kwa kuwa tumezipanga kata kwa tarehe husika kili tupate muda mzuri wa kuwahudumia wananchi, wito wangu waheshimiwa madiwani kuwahimiza wananchi kujitokeza wakiwa na nyaraka husika” alisema Kayombo.

Akichangia Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje alishauri kuwa kliniki hiyo wakati mwingine iwe inakwenda maeneo ya pembezoni kusikiliza kero za Ardhi. “Tunaomba hiyo kliniki iwe inatembea kwa ajili ya kuwafikia wale wasiojiweza katika maeneo ya pembezoni. Wapo wananchi wenye migogoro ya Ardhi ila hawana uwezo wa kufika mjini” alisema Maboje.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma