MAKARANI UCHAGUZI MDOGO KATA YA NALA WAHIMIZWA UADILIFU
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MAKARANI
wa vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Nala,
Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu ili
kufanikisha uchaguzi huo.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo |
Kauli
hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma mjini, John Kayombo
alipokuwa akifungua mafunzo kwa makarani wa vituo vya kupigia kura katika
uchaguzi mdogo wa Kata ya Nala yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kayombo
ambae pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “ninyi
makarani tumewaamini, tumewapa ridhaa muende mkafanye kazi hiyo kwa uadilifu
mkubwa kabisa. Wakati tunawachagua tuliangalia sifa zenu, mliomba wengi.
Mheshimiwa Jaji waliomba watu 1,500 lakini kupata hawa 12 ni mchakato ambao
tumeufanya usiku na mchana mpaka kupata hawa 12 na wa akiba wawili. Siyo kwamba
wale wengine hawana sifa hapana. Sifa moja wapo lazima awe raia wa Taznania,
awe muadilifu, mvumilivu, mwenye hekima, busara, msikivu na anayeweza kufanya
kazi kwa kujituma, tunaamini haya mtakwenda kuyazingatia”.
Akiongelea
kiapo, Kayombo alisema “mmekula kiapo na kwenye zile sifa tumesema asiwe
mshabiki wa chama cha siasa. Chama chako umeshakiacha huko, usiende kushabikia
chama cha siasa, umeshakula kiapo cha kujitoa kwenye chama cha siasa. Umekula
kiapo cha kutunza siri hayo yamekwisha, chochote utakachokwenda kuona kule ni
siri yako, wewe sasa ni mtumishi wa Tume. Kazi yenu nyingine ni kwenda
kuwasaidia wale wapiga kura bila upendeleo wowote wala ubaguzi”.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa,
Mhe. Mwanaisha Kwariko aliwataka makarani hao kutunza viapo vyao. “Hapa mmekula
kiapo, ina maana usipotekeleza yale ambayo umeelekezwa kutekeleza kile kiapo
chako kinaweza kwenda kukufunga. Kwamba umekosea hapa na wakati uliapa
utatekeleza hivi, kwa hiyo unaweza kushitakiwa kwa kile kiapo ulichoahidi na
kushindwa kukitekeleza” alisema Mhe. Jaji Kwariko.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Mwanaisha Kwariko |
Aidha,
aliwataka kutokufanya kazi kwa mazoea. Aliwataka kuona kuwa kila unapofanyika
uchaguzi wajue ni tukio jipya na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea. “Wapiga kura
ndio wateja wetu wa siku hiyo, mteja inatakiwa umpe huduma nzuri, mteja ni
mfalme kwahiyo, wale wapiga kura ni wateja wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa
hiyo tunatarajia kufanya kazi kwa weledi” alisema Mhe. Jaji Kwariko.
Mafunzo
kwa makarani 12 wa vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani Kata
ya Nala yalitolewa ikiwa ni maandalizi kuelekea uchaguzi huo utakaofanyika
tarehe 19 Septemba, 2023.
MWISHO
Comments
Post a Comment