KAMATI YA UJENZI, MANUNUZI NA MAPOKEZI JIJI LA DODOMA ZATAKIWA KUWA NA WATAALAM
Na.
Dennis Gondwe, MIYUJI
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo ameagiza kamati zinazohusika na
ujenzi, manunuzi na mapokezi ya vifaa kuwa na wataalam wa fani husika ili
kwenda sawa na matakwa ya mwongozo wa matumizi ya ‘force account’ katika
kutekeleza miradi ya ujenzi.
Agizo
hilo alilitoa alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari
Miyuji inayojengwa katika Kata ya Miyuji jijini Dodoma.
Kayombo
alisema kuwa mwongozo wa matumizi ya ‘force account’ unaelekeza ziundwe kamati
zenye mchanganyiko wa wajumbe na wataalam. Kamati hizo ni ujenzi, manunuzi na
mapokezi ya vifaa. “Katibu wa Kamati ya Manunuzi lazima awe mtaalam wa Manunuzi.
Lengo ni kuwaongoza wajumbe kwenye taratibu za Manunuzi kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizopo. Kamati ya Ujenzi katibu wake anatakiwa kuwa Mhandisi na Kamati
ya Mapokezi inatakiwa kuwa na mtu mwenye ujuzi wa mapokezi na utunzaji wa
vifaa. Hivyo, maelekezo yangu wataalam hao waingizwe kwenye kamati ili kamati
iwe na ufanisi katika kutekeleza majukumu yake” alisema Kayombo.
Aidha,
alisema kuwa tafsiri sahihi ya kujenga ni pamoja na kutunza taarifa sahihi za
mradi. “Naelekeza kamati za maendeleo zipewe taarifa sahihi na kufikia tarehe
30 Septemba, 2023 mradi huu ukabidhiwe ukiwa umekamilika” alisisitiza Kayombo.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Miyuji, Beatrice Ngerangera alisema kuwa dhamira
ya serikali kujenga shule hiyo mpya ni kuwasaidia watoto wanaotembea umbali
mrefu kufuata shule ili waweze kusoma karibu. “Mimi lengo lango kwa huu mradi
ufike hatua ambayo Rais, Dkt. Samia anataka kwa sababu ni mradi mkubwa na ni
zawadi kwa wananchi wangu wa Kata ya Miyuji. Watoto wanaotoka huku kwenda
kusoma Miyuji ni mbali sana. Kwa hiyo ninatamani hii shule ikamilike mapema
ikiwezekana mwezi Oktoba watoto wanaosoma kule Miyuji waje kuanza kusoma hapa
ndiyo nia yangu na lengo langu kubwa wananchi wangu wa Miyuji” alisema
Ngerangera.
Awali
Mkuu wa Shule ya Sekondari Miyuji, Greyson Maige alisema kuwa shule yake ilipokea
kiasi cha shilingi 544,225,626 kutoka mradi wa kuboresha ubora wa elimu ya
sekondari nchini (SEQUIP) kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari
Miyuji.
Akiongelea
hatua za utekelezaji wa mradi huo alisema kuwa ujenzi wa madarasa mawili yapo
hatua ya ujenzi wa kuta na mawili yapo hatua ya kumwaga jamvi. “Ujenzi wa
madarasa manne yenye ofisi mbili ni darasa moja lipo kwenye hatua ya kupaua na
madarasa matatu yapo kwenye hatua ya kuweka renta. Jengo la utawala tulitenga
siku mbili kwa ajili ya kumwagilia maji na sasa lipo katika hatua ya ujenzi wa
renta ambao unaendeleo leo. Jengo la maabadara ya kemia na baiolojia lipo hatua
ya ujenzi wa renta” alisema Maige.
Majengo
mengine aliyataja kuwa ni maabara ya fizikia iliyopo hatua ya kupanga mawe
katika msingi. “Jengo la maktaba lipo katika hatua ya ujenzi wa renta. Jengo la
Tehama lipo hatua ya ujenzi wa renta. Jengo la vyoo vya wasichana hatua ya
kumwaga jamvi” alisema.
MWISHO
Comments
Post a Comment