RAIS, DKT. SAMIA SULUHU HASSAN ATAKA KULINDA MAADILI YA JAMII
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan amelitaka Kanisa la Anglikana kulinda maadili na kukemea maovu
kwa vijana ili wawe raia wema katika jamii.
Kauli hiyo aiitoa alipokuwa mgeni rasmi katika tukio
la ufunguzi wa jengo la kitega uchumi (Safina house) la Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Central Tanganyika, tukio lililofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Roho
Mtakatifu jijini hapa.
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema “nihimize
kulinda maadili na kukemea maovu katika jamii kwa vijana. Lakini wapo wakubwa
wanaolitumia kanisa kufanya maovu, kemeaneni”.
Aidha, Rais alilipongeza kanisa hilo kwa ujenzi wa jengo
la kitega uchumi (Safina house). “Jengo hili limebadilisha na kuleta mandhari
ya kupendeza kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hii ni hatua moja ya
kujitegemea kwa Dayosisi ya Central Tanganyika. Huduma zilizosubiriwa kwa miaka
sita zimeanza kupatikana. Nimefurahi kuona nembo ya NMB hapa. Serikali imefurahishwa
na kukamilika kwa mradi huu kwa sababu utachangia katika ukuaji wa uchumi na
jamii” alisema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa maelezo ya Askofu na kumkaribisha mgeni rasmi,
Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Mhashamu Dkt. Dickson Chilongani
alisema kuwa jengo la kitega uchumi lilianza kujengwa mwaka 2017. Jengo hilo
liligharimu shilingi bilioni nane. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni mbili ni
msaada kutoka marafiki wa Marekani, shilingi bilioni tatu ni jitihada za ndani
na shilingi bilioni tatu ni mkopo kutoka benki.
Kuhusu usanifu wa jengo hilo, alisema kuwa sura ya
jengo la Safina ni ukumbusho wa Mungu kutumia Safina kumuokoa Nuhu na familia
yake. “Jengo la Safina litumike kuleta wokovu kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na
viunga vyake” alisema Mhashamu Dkt. Chilongani.
Kwa upande wa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary
Senyamule alisema kuwa Mkoa wa Dodoma upo salama na wananchi wanaendelea na
shughuli za kujiletea maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Mkoa wa Dodoma umeanza
kupokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2023 na wanafunzi wote wanapata
sehemu za kulala. Alisema kuwa jumla ya shule 10 mpya zinajengwa katika Mkoa wa
Dodoma za kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.
Akiongelea utekelezaji wa miradi mikubwa, aliitaja
kuwa mradi wa maji wa shilingi bilioni tano unaojengwa katika eneo za Nzuguni
unatarajia kuongeza upatikanaji wa maji kutoka 50% hadi 67%. Mradi wa Barabara
ya Mzuguko, ujenzi wake umefikia 40%. Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Msalato umefikia 20% na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba umefikia 62.5%. “Mheshimiwa
Rais, Mkoa wa Dodoma tunatoa pongezi kwa vipaumbele vyako vinavyogusa maisha ya
watu wa kawaida” alisema Senyamule.
MWISHO
Comments
Post a Comment