Lishe bora yahamasishwa Kliniki ya Magonjwa Yasiyoambukiza Nyerere Square

Na. Nancy Kivuyo, DODOMA

Mamia ya wananchi wamejitokeza kupima afya zao katika kliniki maalum ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuongeza uelewa kuhusu uchunguzi wa mapema, lishe bora na kuzuia magonjwa yanayoendelea kuongezeka nchini.




Taarifa hiyo ilitolewa na Daktari Bingwa wa Afya ya Jamii, Dr. Peter Daud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika bustani ya mapumziko Nyerere Square ambapo maadhimisho ya wiki ya Upimaji Magonjwa yasiyoambukiza yakitamatika.

Dr. Daud alisema kuwa mwamko mkubwa ulioonekana ni ishara kuwa elimu ya lishe na uchunguzi wa mapema inawafikia wananchi kwa ufanisi.
“Sehemu kubwa ya magonjwa yasiyoambukiza inahusiana na lishe. Tunawahimiza wananchi kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi, kula kwa uwiano sahihi na kufanya mazoezi. Hii ni kinga muhimu sana” alisema Dr. Daud.

Aliongeza kwa kutoa wito kuwa wananchi waache tabia bwete kwa kuhakikisha wanafanya mazoezi, kutembea umbali mdogo kwaajili ya kuweka mwili na misuli timamu ili kukwepa maradhi yasiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Makole, Mwendwa Galahenga alisema kuwa kliniki za wazi kama hizo zinawapa wananchi fursa ya kupata elimu ya lishe kila wanapoenda kupima.
“Watu wengi leo wamegundua kuwa ongezeko la uzito na shinikizo la damu linatokana na ulaji usio sahihi. Tunawaelekeza nini kile wanachopaswa kubadilisha kwenye mlo wa kila siku ili wawe na uzito sahihi. Ni jukumu letu sisi wataalam lakini pia wananchi kuwa na mazoea ya kutembelea hospitali, vituo vya afya, kiliniki kama hizi kwasababu watajifunza mambo mzuri na yenye tija kuhusiana na lishe bora” alieleza.




Katika hatua nyingine, Dr. Zaituni Mgaza, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake alisema kuwa upatikanaji wa elimu ya lishe ni nguzo muhimu katika kupunguza hatari ya saratani na magonjwa mengine kwa wanawake. “Lishe bora ni ngao ya kwanza ya afya. Wanawake wakipata elimu sahihi kuhusu nini wanapaswa kula, muda gani wale na namna ya kuchagua vyakula salama tunapunguza maradufu hatari za magonjwa yanayoweza kuzuilika” alisema.

Miongoni mwa waliopata huduma, Joyce Wikezi aliyefanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi alisema kuwa kliniki hiyo imempa nafasi ya kujitokeza kupima magonjwa hayo kabla hajaenda kwenye ngazi zingine. “Nimepata pia elimu ya lishe, jambo ambalo sikuwahi kulielewa vizuri. Wamenifundisha umuhimu wa kula kwa uwiano na kuepuka vyakula vinavyoongeza hatari ya saratani. Nimejifunza mengi” alisema Joyce kwa shukrani.

Kliniki hiyo ilianza tangu tarehe 12 Novemba na kuhitimishwa leo tarehe 14 Novemba, 2025 ambapo wananchi wamepata fursa ya kupima shinikizo la damu, kiwango cha sukari, uzito na urefu, uchunguzi wa magonjwa ya moyo pamoja na ushauri wa kina kuhusu lishe ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya mbogamboga, matunda, ulaji wa vyakula visivyo na mafuta mengi, pamoja na kupunguza sukari na chumvi.

MWISHO

 

 

 

Comments

Popular Posts

Agenda ya Lishe yaongeza Ari ya usomaji S/M Dodoma Makulu

Miaka minne ya Dkt. Samia, Kizota yanufaika mikopo ya asilimia 10

Halmashauri ya Jiji la Dodoma Kuhudumia Majimbo Mawili ya Uchaguzi