Chupa 41 za damu zakusanywa Nyerere Square, wananchi wahimizwa kuendelea kuchangia

Na. Nancy Rogers, DODOMA

Jumla ya chupa 41 za damu zilikusanywa kutoka kwa wachangiaji waliojitokeza kwa hiari katika siku ya kwanza ya Kliniki ya Upimaji Magonjwa yasiyoambukiza inayoendelea katika bustani ya mapumziko Nyerere Square jijin Dodoma.


Uchangiaji huo wa damu umehimizwa kufanyika kila wakati kwa lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu kwa dharura hospitalini, huku wakazi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu la kuokoa maisha.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Timu za Ukusanyaji Damu Kanda ya Kati kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Leah Kitundya ambae alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu mara kwa mara, kwasababu mahitaji ya damu katika hospitali yanaongezeka kila siku. “Tunaendelea kuhimiza jamii kuchangia damu kwa hiari, kwa kuwa damu ni uhai na inaweza kuokoa maisha ya mama wajawazito, wagonjwa wa upasuaji na wa ajali” alisema.

Mmoja wa wachangiaji damu na Mkazi wa Miyuji, Rehema Juma alisema kuwa uchangiaji damu ni tendo la huruma linalookoa maisha. “Mimi niliwahi kuongezewa damu baada ya kujifungua kwa shida, na leo niko hai kwa sababu ya watu waliotoa damu kwa hiari. Kwa maana hiyo nawahimiza wananchi wenzangu kusogea hapa kuchangia damu ili tuwasaidie wengine” alisema.

Nae, Mkazi wa Makole, Emmanuel Mushi ambaye alihudhuria kliniki hiyo, alisema kuwa upimaji wa bure na elimu inayotolewa imewasaidia wengi kuelewa umuhimu wa kuangalia afya zao. “Nilipimwa shinikizo la damu na nimepata ushauri mzuri wa kitabibu. Ni huduma ya muhimu sana kwa jamii, japo sijachangia damu lakini wakati ujao nitachangia ili kugusa maisha ya wengine” alisema.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Agenda ya Lishe yaongeza Ari ya usomaji S/M Dodoma Makulu

Miaka minne ya Dkt. Samia, Kizota yanufaika mikopo ya asilimia 10

Halmashauri ya Jiji la Dodoma Kuhudumia Majimbo Mawili ya Uchaguzi