Watahiniwa 19,176 Darasa IV kupimwa Jiji la Dodoma
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Maandalizi
ya Mtihani wa Upimaji Kitaifa kwa Darasa la Nne (SFNA) utakaofanyika tarehe
22-23 Oktoba, 2025 yamekamilika ambapo Halmashauri ya Jiji la Dodoma yenye
shule 174 kati ya shule 188 za msingi zitashiriki kufanya mtihani huo.
Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Mwl. Prisca Myalla alisema kuwa kati ya watahiniwa 19,176 wasichana ni 9,654 sawa na asilimia 50.4 huku wavulana wakiwa 9,522 ambao sawa na asilimia 49.6
Aliongeza
kuwa maandalizi yote yamekamilika na miundombinu ni rafiki kwa watahiniwa wote.
“Maandalizi yamekamilika, tunasubiri muda ufike ili watahiniwa wetu wafanye
mitihani yao vizuri bila changamoto yoyote. Vituo vyote vitakavyotumiwa ni
salama kabisa kwa mantiki hiyo niwakumbushe wazazi kuwaandaa watahiniwa vizuri
lakini pia nao walengwa wajiandae” alisema Mwl. Myalla.
Nae,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko aliwatakia heri na baraka
watahiniwa wote wa mtihani
huo. Aidha, aliwataka walimu kutekeleza jukumu
la kitaifa
kwa kuzingatia sheria,
kanuni,
taratibu
na miongozo iliyopo ili kulifanya zoezi hilo kukamilika kwa weledi.
Shule 14 ambazo hazitashiriki katika mtihani huo ni shule zenye madarasa ya awali na shikizi ambazo zilijengwa karibu na makazi ya wananchi ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
MWISHO
Comments
Post a Comment