TANZANIA YAENDELEA KUTANGAZA NA KUKUZA KISWAHILI NA UTAMADUNI WAKE KIMATAIFA
Lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania
vimeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali wa kimataifa
waliotembelea banda la Tanzania katika Wiki ya utamaduni na Kiswahili
inayoendelea kwenye maonesho ya biashara ya dunia (Expo 2025) yanayofanyika
Osaka, Japan.
Kuelekea maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani yanayofanyika kila ifikapo tarehe 7 Julai lugha ya Kiswahili inaendelea kuwafikia watu wengi duniani na mwaka huu 2025 maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kiswahili kwa amani na mshikamano”.
Viongozi waandamizi wa mataifa mbalimbali, wametembelea banda
hilo ikiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japani, Bw. Koichiro
Gemba, Mfalme wa Lesotho, Mhe. Letsie III na Mhe. Prudence Sebahizi, Waziri wa
Biashara na Viwanda wa Rwanda.
Viongozi hao wameonesha kuvutiwa kwa kiasi kikubwa na lugha ya
Kiswahili na Utamaduni kupata nafasi katika Maonesho hayo ya Dunia yenye hadhi
kubwa.
Akizungumza wakati alipotembelea banda hilo Mhe. Sebahizi
alieleza kufurahishwa na namna lugha ya Kiswahili ilivyopewa nafasi katika
maonesho hayo ya dunia na kudai Kiswahili kinaweza kuwa nyenzo muhimu katika
kuwaunganisha Waafrika katika juhudi zao za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na
kijamii.
Akizungumza na maofisa wa taasisi za Tanzania zinazoshiriki
katika maonesho hayo, ikiwemo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mhe. Sebahizi amesema kuwa lugha ya
kiswahili inakidhi kwa matumizi miongoni mwa Waafrika
Viongozi hao pia walipata fursa ya kujionea vivutio vya
kitamaduni kama vile mavazi ya jadi, sanaa za mikono, bidhaa za kipekee kama
kahawa ya Kilimanjaro, Madini ya Tanzanite, viungo vya asili vya Zanzibar na
machapisho mbalimbali ya Kiswahili huku Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka BAKITA
ikiwavutia wengi.
Ushiriki huu wa Tanzania katika maonesho hayo ambayo kwa upande
wa Tanzania yanaratibiwa na TanTrade, ni sehemu ya juhudi endelevu za
kuitangaza lugha ya Kiswahili kama urithi wa Afrika na dunia, sambamba na
utamaduni wake tajiri, ili kuimarisha uhusiano ya kimataifa na kuvutia
wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo kupitia nguvu ya lugha na
utambulisho wa kitaifa.
Kilele cha wiki hii ya Utamaduni na Kiswahili katika maonesho
hayo kitafanyika tarehe 7 mwezi wa 7, ambapo kwa kawaida huwa ni Maadhimisho ya
Siku Kiswahili Duniani (MASIKIDU), ambapo kutakuwa na utoaji wa vyeti na tuzo
mbalimbali kwa wadau walioshiriki kwa hali na mali kukikuza, kukieneza, na
kukiendeleza Kiswahili nchini Japani.
Chanzo, The Dodoma Post
Comments
Post a Comment