Shule ya Sekondari ya Bil. 3.9 kujengwa Kata ya Chahwa
Na. Emanuel Charles, CHAHWA
Hafla ya kusaini Mkataba wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Chahwa wenye thamani ya shilingi bilioni 3.9 baina ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Mkandarasi kutoka Gopa contractors Tanzanian Limited imefanyika katika Kata ya Chahwa ukilenga kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi.
Mradi huo unatekelezwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri
ya Jiji la Dodoma ukiwa ni ujenzi wa shule ya ghorofa nne yenye madarasa 12,
maktaba pamoja na maabara nne, chumba cha TEHAMA na jengo la utawala na unatarajiwa
kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Akizungumza katika utiaji saini wa ujenzi wa shule hiyo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alitoa pongezi kwa serikali kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu na kuleta miradi mikubwa katika maeneo ya nje ya Mji wa Dodoma. “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mradi huu mkubwa kwasababu unaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu, ndugu zangu ni wakati sasa maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Dodoma yanufaike na miradi mikubwa kama ilivyokuwa mjini. Tunatamani kuwaona watoto wa Dodoma na Kata ya Chahwa wanayatumia majengo haya kwaajili ya kupata elimu ili waje kuisaidia jamii ya watanzania hiyo ndio imani yetu kubwa na ndio sababu tunasogeza huduma hii” alisema Mavunde.
Aidha, aliongezea kwa kuwaomba wazazi wa Kata ya Chahwa kuwahamasisha watoto wao kusoma kwasababu majengo ambayo yatajengwa sio mapambo bali yatumike katika kutoa elimu. “Haya majengo sio mapambo ndugu zangu tumejenga vyuo vingi ndani ya Mkoa wa Dodoma lakini wanaosoma wengi hawatoki katika mkoa wa Dodoma. Hivyo, basi sisi kama viongozi tunatamani kuwaona watoto wa Dodoma wanatumia miradi hii ya elimu kwasababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya kazi kubwa sana katika sekta ya elimu hivyo basi wazazi muwahamasishe watoto ili waweze kupata elimu” aliongeza Mavunde.
Nae, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliwaasa wananchi wa Chahwa kupendana na kuheshimu taratibu ambazo zimewekwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuweza kuondoa tofauti baina yao. Pia alipongeza Baraza la Madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo kwaajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Chahwa. “Nalishukuru Baraza la Madiwani kwa mkazo uliopo kuhakikisha mapato yanakusanywa na kufikia bilioni 3 ambazo kwa halmashauri nyingine ni bajeti yao ya mwaka lakini sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma bajeti hiyo ambayo kwao ni ya mwaka kwetu itatumika kujenge shule ya sekondari Chahwa. Hivyo basi tutumie fursa hii kuwaleta watoto wetu waje kusoma katika shule hizi” alisema Prof. Mwamfupe.
Halikadhalika Diwani wa Kata ya Chahwa, Sospeter Mazengo
aliipongeza serikali kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu na kuruhusu
mradi huo mkubwa wa shule kujengwa katika Kata ya Chahwa. “Sisi wana Chahwa hii
ni fursa kubwa sana kiuchumi na kielimu kwasababu kupitia mradi huu wananchi
tutanufaika. Pia niwapongeze viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
kuona sisi wana Chahwa tunastahili kuwa na mradi huu mkubwa wa shule ya
sekondari wenye thamani ya shilingi bilioni 3.9” alipongeza Mazengo.
MWISHO
Comments
Post a Comment