Bima ya Taifa ya Afya yatoa huduma kieletroniki

Na. Leah Mabalwe, DODOMA

Maboresho ya huduma ya Bima ya Afya yamefanywa kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia ambapo wananchi wanaweza kujisajili kupata huduma za bima kupitia simu zao na vifaa vya kieletroniki vyenye ‘Internet’.



Hayo yalisemwa na Afisa Wanachama Mwandamizi, Bima ya Afya Mkoa wa Dodoma, Bakary Hamdun katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri wakati akiwasilisha sheria ya afya na kanuni zake.

Alisema kuwa kila mwanachama anaetarajia kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) anaweza kujihudumia kupitia simu ya mkononi “Mwanachama yeyote awe mtumishi au mwananchi wa kawaida anaweza kujisajili kupitia simu yake ya mkononi. Na anaweza kufanya hivyo bila kuwa na changamoto ya aina yoyote kwasababu huduma hii ni rahisi pia inafanyika kwa muda mfupi” alisema Hamdun.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe aliipongeza serikali kwa hatua kubwa ya uboreshaji wa huduma ya Bima ya Afya kwa kutumia vifaa vya kisasa vya kieletroniki.



Alisema kuwa uborehaji huo wa huduma ya bima kupitia simu  janja ni rahisi, pia inaweza kuwafikia watu walio mbali na vituo vya utoaji huduma. “Nipende kuipongeza serikali kwa kufikia hatua hii ya uboreshaji wa kieletroniki kwasababu huduma hii ya Bima ya Afya itasaidia kwa watu waliopo wilaya tofauti tofauti kwa kutumia simu zao za mkononi. Pia suala hili la ukataji wa bima ni muhimu na tulitilie maanani” alisema Prof. Mwamfupe.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri aliwataka wananchi wote kukata Bima za Afya kwasababu taasisi za afya zimekuja na njia rahisi za huduma hiyo.



Aliongeza kwa kuwataka wamiliki wa vyombo vya moto, biashara na majengo kukatia bima ya mali zao ili kuepuka hasara pale ambapo majanga yatakapo kumba mali zao kama ajali ya moto. “Nipende kuwahamasisha wananchi muweze kukata bima hizi kwasabu zinasaidia hata pale unapopatwa na matatizo mfano ajari za barabarani au kuunguliwa na nyumba basi bima uliyoikata itakusaidia iwe hospitali na sehemu yoyote ile ambapo umempata tatizo” alisema Shekimweri.

MWISHO

 

 

 

 

 

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi

RC Dodoma apongeza wafugaji kwa ushiriki wa Paredi ya Mifugo

Rais Samia: Tumieni kikamilifu Miundombinu, Teknolojia na mitaji iliyowekezwa katika Kilimo, Uvuvi na Mifugo