Wanafunzi Hazina Sec watakiwa kufunguka dhidi ya ukatili
Na. Halima Majidi, HAZINA
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Hazina,
iliopo katika Kata ya Hazina, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wametakiwa kuwa
wawazi na wakweli katika kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia ili kuepuka
vitendo hatarishi vitakavyo sababisha kudumaza fikra na ufaulu katika masomo
yao.
Hayo yalisemwa na Afisa Mtendeji wa Kata ya Hazina, Tunu Dachi alipofanya ziara ya utoaji wa elimu juu ya masuala mbalimbali katika kata hiyo.
Alisema kuwa inabidi ziara zifanyike mara kwa
mara za kutoa elimu ili watoto wetu waweze kujitambua waelewe majukumu yao
wakiwa shuleni, waweze kusoma katika mazingira mazuri kiakili na kihisia. “Leo
tumekuja shuleni kama 'normal routine' kwaajili ya kuwatembelea watoto, kuwapa
elimu dhidi ya ukatili kwa ujumla, watoto wamekuwa wakweli wameuliza maswali ambayo
sisi yametupa kazi ya kwenda kuyafanyia kazi na kuwaletea majibu chanya’
alisema Dachi.
Alisema kuwa, anaamini ili mwanafunzi afanye
vizuri sio mpaka awe na majengo na walimu wazuri ila awe tayari kupokea kile
anachofundishwa. “Tumefurahi sana na tumefarijika sana watoto wetu wa shule ya
Sekondari Hazina ni weledi wamechangia
mada, wameuliza maswali tumepata
kufungukiwa mambo mengi ambayo na sisi yametugusa kama walezi wao wa kata”
alisema Dachi.
Aidha, alifafanua kuwa kuhusu masuala ya ulinzi
na usalama yeye kama Mwenyekiti wa Kamati hiyo atahakikisha usalama wao
unaimarika hasa katika mazingira ya shuleni ili waweza kufikia malengo yao. “Naahidi
kuwalinda, usalama wenu utakuwa wa uhakika, endeleeni kushirikiana nasi pale
mtakapopata changamoto ambazo mnahisi haziwezi kupatiwa ufumbuzi hapa shuleni
basi zifikisheni ofisini kwetu. Mimi na idara yangu ya maendeleo ya jamii na wataalamu
wote tutawapa ushirikiano mtakaouhitaji” alifafanua Dachi.
Nae, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Hazina,
Sikujua Mkita, alisema kuwa umuhimu wa kutoa elimu hiyo ni kuwawezesha watoto
kujitambua na kuweza kugundua ukatili wa kijinsia wanaoweza kufanyiwa. “Kuna
ukatili wa aina mbalimbali, na watoto wanafanyiwa ukati nyumbani, njiani na
shuleni, kuna wengine hawawezi kuongea kwenye hadhara. Hivyo, tumeunda baraza
shuleni ili watoto waweze kuwa huru kuripoti vitendo vya ukatili bila kuhofia
mtu yoyote” alisema Mkita.
Kwa upande wake Mwalimu wa Nidhamu Shule ya
Sekondari Hazina, Silvanus Rwechungura, alipongeza wadau akiwemo Afisa Mtendaji
Kata kwa kuwatembelea na kuwapatia elimu hiyo na kama shule bado tunaendelea na
malezi kwa vijana na pia tunashukuru wadau wa elimu Dodoma, kwa kutambua
mchango wetu na tumeweza kupata cheti cha ufaulu wa kidato cha Nne kwa mwaka
2024. “Binafsi kama walimu wa Hazina Sekondari
tumefurahi sana kwa namna ambavyo
wadau wa elimu wametambua mchango wetu, kwa kuangalia cheti kile tumeweza
kutoka nafasi ya 53 Wilaya ya Dodoma mwaka 2023, na kufikia nafasi ya 32 mwaka
2024. Huu ni mchango mkubwa kwa wadau kwa namna ambavyo wanatupa ushirikiano lakini
pia kwa serikali ya awamu ya sita ambayo imeendelea kutoa mchango mkubwa kwa kuwezesha katika mahitaji
mbalimbali” alipongeza Rwechungura.
Atka Kassim ambae ni Mwanafunzi wa kidato cha
Nne, katika Shule ya Sekondari Hazina, alisema kuwa anashukuru kwa elimu dhidi ya
ukatili wa kijinsia, ambayo itawasaidi kutoa changamoto zinazowakabili. “Tunashukuru
kwa elimu hii kwasababu ukatili wa kijinsia katika shule za 'public' huwa ni mkubwa.
Hivyo, inatusaidia kutoa yaliopo moyoni mwetu ambapo tunashindwa kuwaambia
walimu, tunawaambia nyinyi ili muweze kutusaidia kuepuka janga hili la ukatili
wa kijinsia” alisema Kassim.
Mohammedi Naibu Mwanafunzi wa kidato cha
tatu, Shule ya Sekondari Hazina, alisema kuwa mbali na elimu hiyo lakini pia
tunaomba kujengewa maabara, tunashindwa kufanya majaribio kwa vitendo kwa
sababu hatuna maabara. “Maabara imekuwa ni changamoto kubwa, hasa tunaosoma
sayansi tunashindwa kufanya vizuri kwasababu hatuna vifaaa hivyo, tunaomba
mtusaidie” alisema Naibu.
MWISHO
Comments
Post a Comment