Wananchi jijini Dodoma watarajia makubwa Kliniki ya Ardhi
Na. Halima Majidi, VIWANDANI
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanya Kliniki
ya Ardhi ambayo inalenga kutatua changamoto za Ardhi zinazowakabili wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kliniki
hiyo iliofanyi viwanja vya Manispaa ya zamani, Sara Kashaji ambae ni Mkazi wa
Kata ya Ipagala, alisema kuwa awali alikuwa na shamba heka mbili ukanda wa
kijani, ambapo alikuwa anafanya shughuli za kilimo, shamba hilo lilichukuliwa
na Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuahidiwa kupatiwa eneo lingine kwaajili ya
kuendeleza shughuli zake za kilimo.
“Halmashauri walikuja kupima shamba langu,
baada ya zoezi la upimaji waliahidi kutupatia maeneo wakazi wa eneo hilo, baada
ya hapo tulihama na kuachia vijiji vile na kwenda sehemu nyingine, Kamishna
alisema mashamba yale kuna watu wamepewa. Hivyo, sisi tusubiri kupimiwa eneo
lingine Kikombo ambapo tulivyofika kule wananchi walikataa maeneo hayo,
tukaambiwa tusubiri kupimiwa Makulu na mpaka sasa sijapata ufumbuzi” alisema
Kashaji.
Aidha, alifafanua kuwa kero yake kubwa ni
kurudishiwa maeneo yake kwa sababu ni muda mrefu tangu ameanza kufuatilia
shamba hilo. Alimuomba Kamishna wa Ardhi awaangalie kwa jicho la huruma. “Nimehangaika
kwa miaka mingi tangu niahidiwe kupewa mbadala wa shamba lile na tumekuwa
tukiahidiwa kupimiwa maeneo hayo lakini mpaka sasa sijapata muafaka” alifafanua
Kashaji.
Aliongeza kuwa kutokana na Kliniki ya Ardhi,
anatarajia kupata ufumbuzi wa changamoto yake kwa kupatiwa eneo lingine
kwaajili ya kuendeleza shughuli zake za kilimo ili kuweza kujikwamia kimaisha
na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. “Mpaka sasa tunatembea hatujapata majibu tunaambiwa
bado wanapima. Leo tumetegemea kumkuta kamishna ili tumpatie karatasi zetu
kwaajili ya kupata viwanja vyetu, hayo ndio matarajio yangu” aliongeza Kashaji.
Kwa upande wake Selina Mkami, Mkazi wa Kata
ya Ipagala alisema kuwa kwa mara ya kwanza alivyoenda na mpimaji alipata
matumaini ya kupata eneo lake lakini chakusikitisha hadi leo bado anahangaika. Hivyo, anaomba mamlaka
husika itutae changamoto hiyo. “Nimetembea na nimehangaika kwa muda mrefu bila
kukata tamaa ili kuona napata eneo langu, na kinachonisikitisha zaidi nikwamba
sisi tulitolewa kwenye maeneo yetu na tukaacha kulima wakawekwa watu wengine
kwa kweli inaniuma sana” alisema Mkami.
Nae Msimamizi wa Upimaji wa Ardhi wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Hassan Muhsin alisema kuwa ili waweze kuhudumia wananchi kwa
pamoja waliona upo umuhimu wakuandaa kliniki hiyo kwa kuhakikisha wananchi wanapata
ufumbuzi katika masuala ya Ardhi. “Kwa kushirikiana na vitengo husika leo
tutahakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki na tunashukuru wananchi
wameonesha muitikio na niwaombe wananchi wawe wawazi, wakweli na uthibitisho. Sisi
tumejipanga vizuri katika kuhakikisha tunatatua matatizo yao” alisema Muhsin.
Kliniki ya Ardhi Halmashauri ya
Jiji la DOdoma imeanza tarehe 25 na itaendelea hadi tarehe 28 Februari 2025,
ikiwa na lengo la kutatua changamoto za ardhi zinazowakabili wananchi.
MWISHO
Comments
Post a Comment