Walimu wakuu Jiji la Dodoma kupatiwa Mafunzo ya NeST
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Walimu
wakuu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamepatiwa mafunzo juu ya ununuzi
kwa njia ya mtandao serikalini yatakayoboresha utendaji kazi na kuwawezesha
kupata mafundi na watoa huduma kupitia mfumo wa ununuzi ‘National
e-Procurement System of Tanzania’ yaani ‘NeST’.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero akifungua Mafunzo ya Ununuzi kwa njia ya Mtandao (NeST)
Mafunzo
hayo yameanza leo tarehe 21 Januari, 2025 na Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa walimu wakuu wa shule za msingi katika
ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi, Vincent Odero alisema kuwa mfumo wa
manunuzi serikalini kwa njia ya kielektroniki ni mfumo mzuri na umerahisisha
mchakato mzima wa manunuzi na umeleta ufanisi mkubwa katika ununuzi wa umma
katika maeneo mbalimbali. “Mfumo huu ni mzuri, umerahisisha mchakato wa ununuzi
ambapo taratibu zote za ununuzi hufanyika ndani ya mfumo. Mfumo huu umeleta
ufanisi katika ununuzi wa umma kupitia maeneo mbalimbali” alisema Odero.
Kuhusu
umuhimu wa mfumo wa ununuzi serikalini, alieleza namna ambavyo mfumo
umerahisisha utendaji kazi tofauti na mfumo uliokuwa unatumika awali. “Mfumo wa
ununuzi umeongeza uwazi na usawa katika mchakato wa ununuzi, kila mzabuni ana
haki sawa ya kuwasilisha zabuni na umepunguza muda wa mchakato wa zabuni. Hivyo,
kusaidia ununuzi kufanyika kwa muda mfupi, umepunguza mianya ya rushwa,
umeboresha utunzaji wa taarifa za michakato ya ununuzi, umeongeza uwajibikaji
kwa watumishi wa umma kwasababu mfumo unaonesha kila hatua ya ununuzi na
kupunguza gharama za michakato ya zabuni kwa taasisi na wazabuni” alisisitiza Odero.
Sanjari
na hayo alielezea kuhusu agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Waraka wa Hazina Namba 2 wa Mwaka 2023/2024, alisema kuwa, unaelekeza
watumishi wote wa umma wanahusika na mchakato wa ununuzi ndani ya taasisi za
serikali kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha watumishi kutumia mfumo wa NeST kwa
ufasaha. “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 27 Julai,
2023 ilitoa Waraka wa Hazina Namba. 2 wa Mwaka 2023/24 kuhusu matumizi ya mfumo
wa usimamizi wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielekroniki ‘NeST’, ambao
ulielekeza kwamba, watumishi wote wa umma wanahusika na mchakato wa ununuzi
ndani ya taasisi za serikali wapewe mafunzo yatakayowawezesha kutumia mfumo kwa
ufasaha. Halmashauri ilitekeleza jukumu hilo kwa kuwawezesha maafisa ununuzi na
ugavi kupata mafunzo hayo” alisema Odero.
Aidha,
aliwataka walimu wakuu kutokiuka sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Mamlaka
ya Udhibiti na Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA). “Kaguzi za Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA)
zinazofanyika kila mwaka, zimebaini kuwepo kwa mapungufu katika taratibu za
ununuzi unaofanyika ikiwemo ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo
inayotolewa. Mapungufu haya yamekuwa ni sababu kubwa ya upotevu wa fedha za
serikali na miradi mingi kushindwa kukamilika na iliyokamilika kutokuwa na
ubora unaotakiwa. Hivyo, niwaombe kufuata kanuni na taratibu zinazotolewa na
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Unuuzi wa Umma (PPRA) alisisitiza Odero.
Mkuu
huyo wa kitengo alisema kuwa katika mafunzo hayo washiriki watafundishwa
kuandaa mpango wa ununuzi wa mwaka, kuanzisha manunuzi kwenye mfumo, kuandaa
nyaraka za zabuni kwenye mfumo. Maeneo mengine ya mafunzo aliyataja kuwa ni
kufanya ufunguzi wa zabuni kwenye mfumo, kufanya tathmini kwenye mfumo, kutunuku
zabuni kwenye mfumo na kuandaa mkataba kwenye mfumo, aliongeza.
Vilevile,
aliongeza kwa kusema kuwa, watumishi hao wameaminiwa na kukabidhiwa na serikali
jukumu la kufanya na kusimamia ununuzi wa umma katika vituo vyao vya kutolea
huduma. Pia alisema kwa atakaekiuka sheria na kanuni hatua kali za kisheria
zitachukuliwa ikiwa ni faini ya shilingi 10,000,000 kwenda jela miaka mitatu au
vyote kwa pamoja.
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma imeandaa mafunzo kwa mara nyingine kwa watumishi wote
kutokana na maelekezo ya serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) kwa halmashauri zote nchini kutumia ‘NeST App’ kwa manunuzi
yote yanayofanyika ofisi kuu na katika vituo vya kutolea huduma.
MWISHO
Comments
Post a Comment