Kata ya Mkonze yabainisha watoto wenye mahitaji maalum kupata elimu
Na. Coletha Charles, MKONZE
Halmashauri ya
Jiji la Dodoma imeendelea na zoezi la kubainisha watoto wenye mahitaji maalum
kwa lengo la kujiunga na elimu ya awali na msingi kwa mwaka 2025, kwa
ushirikiano na viongozi wa kata, mitaa na wazazi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkonze, Herieth Reuben, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum kupata fursa za kielimu na kijamii zinazolingana na mahitaji yao.
Alisema kuwa kata
hiyo ina wakazi 41,000, mitaa nane na shule 12 za msingi. Hivyo, wamejipanga
kusimamia shughuli ya uandikishaji kwa asilimia 100 na watapita kila kaya
kuwabainisha watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kuanza masomo yao. “Hii ni
sehemu ya mpango wetu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata haki zao za
msingi bila ubaguzi, tunaomba wazazi watupe ushirikiano ili tuweze kuboresha
maswala ya elimu. Lakini pia watoto wengi wenye mahitaji maalum watapata huduma
stahiki, watajiunga na elimu ya msingi kwa sababu kata yetu tumewaandikisha na
tunaendelea kuwaandikisha” alisema Reuben.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkonze, Saidi Waziri, alitoa pendekezo kwa Jiji la Dodoma kuweza kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum shule kwa kutoa taarifa kupitia makanisa na misikiti. “Shule yetu ni jumuishi inachukuwa watoto wa kawaida na wenye mahitaji maalum. Hadi sasa tuna watoto wenye uhitaji maalum wapatao 18, ambao wanaendelea kusoma, lakini leo tumeandikisha watoto watatu ambao watajiunga na darasa la kwanza” alisema Mwalimu Waziri.
Nae, Mwenyekiti wa
Mtaa wa Chidachi, Kata ya Mkonze, Mohamedi Missanga, alimshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea vyumba vya madarasa 16 kwa muda
wa miaka miwili. “Wazazi wapate ushawishi wa kuwapeleka watoto shule na
wawalete waandikishwe. Tutahakikisha tunawatafuta na kuwabaini watoto wote
wenye mahitaji maalum, nyumba kwa nyumba, tukishirikiana na mbunge, madiwani, viongozi
wa mashina na tutawabaini wale wote ambao watakuwa wamewaficha watoto ili
serikali ya awamu ya sita iwashughulikie” alisisitiza Missanga.
Kwa ujumla, zoezi
hilo limelenga kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata nafasi sawa ya kufikia ndoto
zake, huku ikisisitizwa umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa jamii na serikali
katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum.
Habari
hii imehaririwa na John Masanja na Faraja Mbise
MWISHO
Comments
Post a Comment