Dodoma Jiji U20 yatuma salamu Ligi ya Vijana

Na Mussa Richard, DODOMA

 

Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji chini ya umri wa miaka 20 imetuma salamu kwa timu zinazoshiriki ligi ya vijana ya NBC chini ya miaka 20 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Tabota United chini ya miaka 20 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri Dodoma hapo jana.





Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha mkuu wa timu hiyo, Chido Jeremiah alisema “tunamshukuru Mwenyezi Mungu mchezo umeisha salama na tumepata ushindi wa magoli mengi na ushindi wa kutuheshimisha na kutuweka mbele zaidi na wanaotufuata. Japo hatukua na mchezo mzuri kipindi cha kwanza lakini wakati wa mapumziko tukawapa vijana maelekezo ya kufanya kutokana na mapungufu tuliyoyaona kwa wapinzani wetu ndiyo maana tuliporudi kipindi cha pili tukafanikiwa kupata mabao manne. Kwa upande wa timu imeendelea kuimarika na vijana wameanza kujituma na niwashukuru mashabiki wamejitokeza kuiangalia timu yao na wameona jinsi inavyocheza. Kwahiyo, niwaombe wanadodoma wasiiache timu hii timu ni yao na waendelee kuiunga mkono ili iweze kufanya vizuri zaidi” alisema Jeremiah.

Kwa upande wake Bakari Mondwe ambaye ni nahodha wa timu hiyo baada ya mchezo kumalizika alisema “mchezo umeisha, tumepata alama tatu ambazo zimetufanya tuendelee kuwa kileleni kwenye kundi. Malengo yetu katika huu mzunguko wa pili ni kuhakikisha tunamaliza vinara katika kundi na tunavuka katika hii hatua kuingia katika hatua inayofuata na niwaombe mashabiki waendelee kuja kwa wingi kwenye kila mchezo tunaocheza na sisi kama wachezaji jukumu letu ni kuwafurahisha kwa kushinda kila mchezo ulio mbele yetu” alisema Mondwe.

Baada ya ushindi huo Dodoma Jiji U20 ijikita kileleni katika kundi A ikiwa na Alama 16 baada ya kushuka dimbani katika michezo saba ikishinda michezo mita ikitoa sale mchezo mmoja na ikipoteza mchezo mmoja, ikifunga mabao 15 ikifungwa mabao matano pekee ikiwa mbele kwa alama tatu dhidi ya wapinzani wao wanaofuatia ambao ni Azam U20 wenye alama 13. Mchezo unaofuata Dodoma Jiji U20 itashuka dimbani Januari, 22 kuikabiri Mashujaa U20 katika uwanja wa Jamhuri Dodoma ikiwa ni muendelezo wa mbilinge mbilinge za duru ya pili ya Ligi ya Vijana ya NBC Tanzania Bara.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma